WITO umetolewa kwa washiriki wote wa
Mkutano wa Kumi wa Maendeleo ya Takwimu Afrika kuelendelea kutoa takwimu sahihi
na kwa wakati ili kuleta maendeleo yanayokusudiwa ya kiuchumi na kijamii barani
Afrika.
Wito huo umetolewa jana na Waziri
Mkuu wa Uganda Mhe. Dkt. Ruhakana Rugunda wakati akifungua Mkutano wa Kumi wa
Maendeleo ya Takwimu Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Speke
Munyoyo Kampala, Uganda.
Dkt. Rugunda amesema kuwa, ili
kupata maendeleo kwa haraka, ni lazima takwimu zitolewe kwa wakati na ziwe
sahihi kwa ajili ya kusaidia kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.
"Ili Bara la Afrika liweze
kuendelea kwa haraka, linahitaji takwimu sahihi na zinazotolewa kwa wakati ili
takwimu hizo zisaidie katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo",
amesema Waziri Mkuu Rugunda.
Dkt. Rugunda ameongeza kuwa ili
kuweza kufanikisha hilo, kuna umuhimu kwa nchi za Afrika kusaidia program
mbalimbali za uzalishaji wa takwimu na matumizi yake kwa ajili ya kupanga
mipango ya maendeleo.
Kwa upande wa Waziri wa Fedha wa
Uganda Matia Kasaija amesema kuwa, ili kuweza kulinganisha takwimu za nchi
mbalimbali, ni vyema takwimu zinazozalishwa zikafuata mbinu bora za uzalishaji
wa takwimu.
Matia Kasaija amesema mbinu bora za
uzalishaji wa takwimu ni zile zinazofuata viwango vinavyopendekezwa na
Umoja wa Kimataifa - Kitengo cha Takwimu.
Mkutano wa Kumi wa Maendeleo ya
Takwimu Afrika umewakutanisha washiriki takribani 400 kutoka nchi mbalimbali za
Afrika ikiwemo Tanzania. Mkutano huu ni wa siku tatu na unatarajia kumalizika
kesho tarehe 15 Januari, 2015.
Na Mwanaharakati.

No comments:
Post a Comment