WAKAZI wa kijiji cha Nkome wilayani
Geita, wameamua kutelekeza nje ya kituo cha polisi Nkome maiti ya kijana mmoja
anayesadikiwa kupigwa na baadhi ya watu.
Tetesi zinasema kuwa kifo hicho
kimetokea ndani ya kituo hicho na kusababisha kifo chake.
Aliyeuawa ametambulika kuwa ni Mlangila Tigamanywa(22), mkazi wa mtaa wa Yakaranda,kijiji cha Nkome Tarafa ya Bugando wilayani hapa.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nkome Anjero Daniel,amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba lilitokea Desemba 19 mwaka jana majira ya usiku muda mfupi baada ya mzazi wa kijana huyo Bigamanywa Mlangila kumfikisha mwanaye huyo lkituoni hapo.
Akielezea tukio hilo,kaka wa
marehemu,Galindi Lukanazya(35), aliliambia Tanzania Daima kuwa nduguye alipigwa
na askari wawili wa kituo hicho aliowataja kwa majina ya PC Simon na mgambo wa
kituo hicho Mashaka Desemba 19,2014.
Alisema,mdogo wake baada ya
kufikishwa kituoni hapo na baba yake mzazi akiwa na afya njema majira ya jioni
aliwekwa rockup na baadaye baba yake aliondoka kituoni hapo akitakiwa afike
kesho yake kwa ajili ya kuchukuliwa maelezo.
Hata hivyo,majira ya saa 2
usiku wakati mkuu wa kituo hicho Gwaga Mtawa akiwa amekwenda kuangalia taarifa
ya habari kwenye kumbi za starehe Mgambo na askari huyo walimtoa mdogo wake
huyo Rockup na kuanza kumpiga hadi akazirai na kumrejesha tena rockup.
Kwa mjibu wa Lukanazya,baba wa
marehemu alifikia hatua ya kumpeleka polisi mtoto wake huyo baada ya kuvunja
dirisha la nyumba yao hali iliyomchukiza na kuamua kumfikisha kituo cha polisi.
‘’Ni kwamba,baba aliweka
mpangaji kwenye chumba alichokuwa analala marehemu,marehemu akamuuliza baba
yake kama anaweka mpangaji yeye atalala wapi na baba yake alimjibu atafute pa
kulala kwani nyumba ni yake’’
‘’Baada ya baba kumjibu
hivyo,marehemu alikasirika na kuamua kubomoa dirisha la chumba hicho na ndipo
baba yake al;ipokwenda kutoa taarifa polisi ambao walifika na kumkamata na
waliokuja kumkamata ni mgambo huyo na polisi Simon’’
Hata hivyo alisema,wakati
walipokuja kumkamata marehemu hakukubali na walitumia nguvu lakini njia nzima
walikwenda wakitukanana kati ya mgambo,polisi na marehemu na ndiyo sababu za
kumpiga.
‘’Baada ya kukaidi amri ya askari hao,walimchukua kwa nguvu na njia
nzima walikuwa wakitukanana,Kitendo hicho kiliwaudhi askari na mgambo huyo na
walivizia mkuu wa kituo hayupo na ndipo walipomtoa sero na kuanza kumshambulia
kwa kipigo hadi akazirai huku akivuja damu masikioni na kumrudisha tena
sero’’alisema Lukanazya.
Kutokana na kipigo
hicho,Mlangila alijeruhiwa vibaya na siku iliyofuata desemba 20 alipelekwa
katika zahanati ya Nkome kwa matibabu zaidi na baadaye siku hiyohiyo
alihamishiwa katika kituo cha afya cha nzera.
Hata hivyo, baada ya hali ya Mlangila kuonekana kuzidi kuwa mbaya, desemba 24 walilazimika kumhamishia hospitali ya wilaya ya Geita,hadi desemba 31 walipomhamishia katika hospitali ya misheni Sengerema.
Hata hivyo,hali yake ilizidi
kuwa mbaya na Januari 4,2015 waliamua kumhamishia katika hospitali ya rufaa ya
Bugando ili kupata huduma zaidi kabla ya kukumbwa na mauti hayo Januari 9,mwaka
huu.
Hata hivyo katika hali
isiyokuwa kawaida,mwili wa marehemu ambao uliwasili jana nyumbani kwao Nkome
kwa ajili ya mazishi umechukuliwa leo na kwenda kutelekezwa nje ya kituo kidogo
cha polisi cha Nkome baada ya kuwepo kwa tetesi kwamba jeshi la polisi
limepanga kuwalinda watuhumiwa hao na kumtoa kafara mzazi wa mtoto huyo ambaye
tayari anashikiliwa akihusishwa na mauaji ya kijana huyo.
Na VALENCE ROBERT, GEITA
No comments:
Post a Comment