Dada wa msanii mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva,
Seleman Msindi Afande Sele Zaria Kambi (30) ambaye alikuwa ni mhudumu
wa baa, amekutwa ameuawa kikatili katika Gesti ya Stavi (Gesti ya
Marafiki) iliyopo Kichangani, mjini Morogoro.
Tukio hilo la kinyama lilitokea usiku wa Jumapili iliyopita baada ya
marehemu kuwa amekubaliana kulala pamoja na mteja aliyekuwa akimhudumia
kinywaji, ambaye pia alikuwa amechukua chumba katika nyumba hiyo hiyo
iliyokuwa na baa.
Kwa mujibu wa rafiki wa marehemu, ambaye pia alikuwa ni mhudumu wa
gesti hiyo, Rehema Saleh, alisema mtu mmoja asiyefahamika, alifika
kazini kwao na kupanga chumba namba 8A na baadaye alienda upande wa baa
kunywa pombe akihudumiwa na Zaria.
Mimi na Zaria (pichani) tunaishi jirani, sasa baada ya kumhudumia na
yeye kununuliwa pombe, wakakubaliana walale pamoja, tunaishi jirani
hivyo kila siku baa ikifungwa tunaongozana na jana tuliongozana njiani
aliniambia amepata kichwa hivyo anakwenda nyumbani kuaga na baadaye
arejee kwa bwanake huyo ambaye ni mara ya kwanza anaonana naye,
alisema Rehema na kuongeza.
Cha ajabu saa 8 usiku napigiwa simu na mlinzi akidai Zaria
amenyongwa na mteja wake, sikuwa na jinsi, kulipokucha nilifika hapa
gesti na kukuta mwili wa marehemu ukiwa kitandani, alisema na kuangua
kilio
Mlinzi wa gesti hiyo, John Emmanuel akizungumzia tukio hilo, alisema
majira ya saa 6 usiku Zaria aliingia katika chumba namba 8A na saa moja
baadaye, akasikia kelele zikitoka chumbani humo, ambazo alihisi ni za
kimapenzi
Sijakaa vizuri saa 8 usiku jamaa alitoka na begi lake akitaka
nimfungulie aondoke huku mkononi akiwa na tiketi ya basi kuelekea Mbeya,
nikamwambia kwanza twende chumbani kwake nikachunguze ndipo nimruhusu
atoke, awali aligoma na mimi nikagoma kumfungulia geti, tukaganda kama
dakika mbili akakubali kwenda chumbani tulipofika tukamkuta Zaria
amekufa huku akiwa mtupu, nikamjulisha bosi Pascal Mafikiri ambaye
aliita polisi wakamchukua mtuhumiwa na mwili wa Zaria, alisema.
Mama mzazi wa marehemu, Mwajuma Hassani Kambi ambaye ni Mjumbe wa
Serikali ya Mtaa wa Mwande Kata ya Kichangani kwa tiketi ya Chadema
alipokea taarifa za kifo cha mwanaye Jumapili usiku
Alisema mwanaye ameacha mtoto anayeitwa Rashid lsmail Kaliembe ambaye
anasumbuliwa na uvimbe tumboni na kwamba kila mwezi alikuwa akipelekwa
Muhimbili kwa matibabu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtuhumiwa, Erick Bruno, ambaye ni mkazi
wa Manzese Tip Top Dar es Salaam, anashikiliwa. Marehemu huyo alizikwa
Jumanne iliyopita mjini Morogoro.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment