MKUU wa Wilaya ya Kinondoni , Paul
Makonda (pichani) amesema wanaobeza uwezo wake kiutendaji baada ya kuteuliwa na
Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo, wasubiri waone atakavyokuwa.
Aidha, ameweka wazi kile anachoamini
anashutumiwa na kubezwa na watu kuhusu uteuzi huo na kusema wanaofanya hivyo,
wanafahamu kwamba masuala yao kadhaa ndani ya wilaya hiyo yanayokwenda kinyume
na taratibu, hayatafanikiwa.........
Akiendelea kujibu wanaoshutumu
uteuzi wake kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, alisema kwa sasa
hawezi kutoa ahadi ni nini atafanya isipokuwa, anasubiri kuingia ofisini.
Akihojiwa katika kipindi cha asubuhi
cha Redio ya Clouds, alisema pia anamsikiliza Rais atakachomwambia afanye kwa
kuwa yeye ni mwakilishi wake wilayani humo.
Akizungumzia kuhusu taarifa za
kupata nafasi hiyo kuwa gumzo katika jiji kuliko wakuu wengine wa wilaya,
alisema inaonesha ni kwa jinsi gani watu wanatambua utendaji wake.
Alisema alipata taarifa za uteuzi
huo wakati akitoa mada katika kikao cha kazi cha Umoja wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi (UVCCM) na kushangaa watu wakipeana taarifa.
“Kuna watu wanabeza uteuzi wangu kwa
kuonekana nimepewa wilaya kubwa. Nataka kuwaambia wasubiri waone tu,” alisema
na kutaka Watanzania kuacha tabia ya kumjadili mtu au jambo bila kufahamu
vizuri.
Alisisitiza kuwa Watanzania wamekuwa
na tabia ya kushabikia jambo wasilolijua au mtu wasiyemjua kwa kufuata mkumbo;
jambo ambalo siyo zuri ni vyema kufahamu kwanza ndipo uweze kusema.
Akizungumzia baadhi ya vyombo vya
habari vilivyotoa taarifa za uteuzi wake kwa kumdhihaki, alisema wamefanya
hivyo kwa maslahi yao ya kuuza.
Pia alielezea uteuzi wake umekuwa
gumzo, kutokana na uwezo wake wa kazi katika UVCCM pamoja na uwezo wake kwenye
Bunge Maalumu la Katiba.
Uteuzi wa Makonda ambao umefanywa na
Rais Kikwete, unaonesha kuwashitua wengi; hali ambayo imefanya watu wengi
kumbeza hasa kupitia mitandao ya kijamii.
Baadhi ya wanaobeza, wanadai kwamba
Makonda hana sifa ya kuongoza wilaya kubwa kama Kinondoni, ambayo ina
changamoto na migogoro mingi ya ardhi.
Makonda ambaye ni Katibu wa
Chipukizi na Uhamasishaji wa UVCCM, jina lake limekuwa kubwa hivi karibuni
baada ya kutuhumiwa kushiriki kuvuruga mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya
Mwalimu Nyerere, tuhuma alizokanusha.
Pia, kujitokeza kwake hadharani
kumpinga mmoja wa watu wanaotajwa kuwania urais, kuliongeza jina hilo kuwa
maarufu. Maisha ya Makonda pia ambaye baada ya kushindwa Umakamu Mwenyekiti wa
Taifa wa UVCCM, alitoa shutuma kuhusu uchaguzi huo na baadaye alirejeshwa ndani
ya umoja huo kwa kupewa nafasi anayoshikilia sasa ya ukatibu wa uchipukizi na
uhamasishaji.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment