MAC PRODUCTION STUDIO'S

MAC PRODUCTION STUDIO'S
KWA MATANGAZO YA BIASHARA REDIONI( 0767-814844)

Friday, 27 February 2015

TAARIFA INASEMA KUWA WASHITAKIWA WA CUF WAMEZIDI POLISI UJANJA

HATI ya kuwafutia mashtaka wafuasi 30 wa Chama cha Wananchi (CUF) waliotakiwa kuunganishwa katika kesi moja na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba, imezua sintofahamu baada ya wafuasi hao kutoweka.

Wafuasi hao waliotakiwa kuachiwa na kukamatwa tena walitoweka jana katika.............
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru, baada ya kukubali maombi ya kuwaachia huru yaliyowasilishwa na DPP.

DPP aliwasilisha hati ya kuomba washtakiwa hao waachiwe huru (nolle prosequi) kwa madai kwamba Jamhuri haina nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.

Hati hiyo iliwasilishwa chini ya kifungu cha sheria ya makosa ya jinai namba 91(1) na mahakama ilikubali kuwaachia huru.

Jamhuri iliomba kufanya hivyo kwa lengo la kuwaunganisha katika kesi moja na Profesa Lipumba, lakini hawakuweza kufanya hivyo kwa sababu washtakiwa mara baada ya kuachiwa hawakukamatwa tena, walitoweka katika eneo la mahakama bila kusubiri usafiri wa mabasi wanayotumia kila wanapofika hapo.

Wakati watuhumiwa hao wameshatoweka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, aliiomba mahakama kumbadilishia hati ya mashtaka Profesa Lipumba kwa kuwaongeza washtakiwa wengine 30.

Kweka alipokuwa akiwasilisha hoja hiyo, tayari washtakiwa hao walishatoweka katika eneo la mahakama, aliyebakia ni Profesa Lipumba na wafuasi wengine wa kawaida waliofika kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.

Hata hivyo, Wakili Peter Kibatala anayemtetea Profesa Lipumba, alipinga kubadilishwa kwa hati hiyo, akidai waliwasilisha pingamizi la awali dhidi ya mashtaka hayo.

Kibatala alidai miongoni mwa hoja za pingamizi ni kuhusu uhalali wa hati ya mashtaka na mamlaka ya mahakama kusikiliza kesi hiyo.

Alidai kutokana na mapingamizi hayo, mahakama haiwezi kukubali kubadilisha hati hiyo ya mashtaka.
Hata hivyo, Kweka alidai mabadiliko ya hati hiyo ni kuwaongeza washtakiwa na si kubadili kitu kingine chochote.

Hakimu alikubali kumuunganisha Profesa Lipumba na wenzake 30 ambao hawakuwapo mahakamani na Jamhuri waliomba hati ya wito kwa washtakiwa walitoweka ili wafike mahakamani Machi 23, mwaka huu.
Washtakiwa walioachiwa huru na kutoweka ni Shaabani Ngurangwa, Shabani Tano, Shabani Abdallah, Juma Mattar, Mohammed Kirungi, Athumani Ngumwai, Shweji Mohammed, Abdul Juma, Hassan Saidi, Hemed Joho, Mohammed Mbaruku na Issa Hassan.

Wengine ni Allan Ally, Kaisi Kaisi, Abdina Abdina, Allawi Msenga, Mohammed Mtutuma, Salehe Ally, Abel Hatibu, Bakari Malya, Abadallah Ally, Said Mohammed, Salimu Mwafisi, Salehe Rashid, Abdallah Said, Rehema Kawambwa, Salma Nduva, Athumani Said, Dickson Leason na Nurdin Msati.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani Januari 29, mwaka huu wakikabiliwa na mashtaka matatu. Inadaiwa Januari 27, mwaka huu, katika ofisi ya CUF Temeke Hospitali, walikula njama, walikusanyika isivyo halali kwa nia ya kuandamana kwenda Mbagala.

Katika shtaka la tatu washtakiwa wanadaiwa siku hiyo ya tukio waligoma baada ya kutolewa makatazo halali maeneo ya Mtoni Mtongani walipokuwa wamekusanyika.

Profesa Ibrahim Lipumba katika hati yake ya mashtaka anadaiwa Januari 22 na 27, katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam aliwashawishi wafuasi wake kutenda makosa hayo ya jinai.
Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

No comments: