MBUNGE wa Kasulu Mjini, Moses
Machali (NCCR-Mageuzi), ametangaza rasmi kwamba hatagombea tena ubunge wa jimbo
hilo wakati wa uchaguzi mkuu mwaka huu.
Amesema ingawa alikuwa na nia ya
kuendelea kuongoza jimbo hilo, amelazimika kuacha kwa kuwa baadhi ya viongozi
wa chama chake wilayani Kasulu wanachafua jina lake bila sababu...........
Machali alitangaza msimamo huo juzi
mjini Kasulu alipohutubia mkutano wa hadhara.
“Kuna baadhi ya viongozi wachache
wenye mawazo ya kijinga wanaotoka Jimbo la Kasulu Vijijini wanashirikiana na
Diwani wa Kata ya Kasulu Mjini, Issack Rashid maarufu kama Mkemwema,
kunitangaza kwamba nimechukua uamuzi huu kwa sababu Mkemwema anataka kugombea
ubunge katika jimbo langu.
“Hiyo siyo kweli, ugomvi wangu
mkubwa na hao watu umekuja kwa sababu ninapiga vita ufisadi na mafisadi waliopo
Wilaya ya Kasulu wanaojali masilahi yao badala ya wananchi.
“Mimi sipendi usumbufu na wananchi
ingawa wengine wanatembea huku na huko wakisema ‘Machali hatujali’… hivi
mnafikiri atatokea mbunge atakayemaliza shida zenu zote?
“Kama atatokea huyo mbunge basi
njooni mniombe silaha yangu mnipige risasi nife kwa sababu naamini mbunge huyo
hayupo na hatatokea katika dunia hii.
“Watu wananipiga vita bila sababu
kwa vile napingana nao, yaani wanataka na mimi nipige madili kama wao, hiyo
haiwezekani kwa sababu siko tayari kuchafua jina langu.
“Wananisingizia mambo ya uongo, kama
tatizo ni ubunge, basi nimeamua sitagombea ili historia ije inihukumu kwa
sababu ninapopinga ufisadi, mafisadi na watu wa shetani wananipinga,” alisema
Machali.
Hata hivyo, baada ya mbunge huyo
kutoa kauli hiyo, alikumbana na upinzani mkali baada ya baadhi ya wananchi
kupingana naye huku baadhi wakilia.
Baadhi ya wananchi hao walisikika
wakisema hawako tayari kukubaliana na mbunge huyo kwa kuwa wanaridhishwa
utendaji kazi wake.
“Usiache kugombea maana wewe ndiyo
kimbilio letu kwa sababu umetusaidia katika maeneo ya Kagerankanda wakati
tulipokuwa tukinyanyaswa na Mkuu wa Wilaya mstaafu, Dan Makanga.
“Wewe ulisimama na sisi na leo
Makanga hayupo tena, kwa hiyo, kama usipogombea sisi wanyonge tutatetewa na
nani,” walisikika baadhi ya wananchi wakisema.
Baada ya wananchi hao kusema hayo,
Machali alisimama tena na kuomba apewe muda atafakari maombi yao.
“Naomba nipewe muda wa kutafakari,
wazee wangu nimewasikia, vijana wenzangu nimewasikia na akina mama nimewasikia
pia. Niacheni nitafakari kwa sababu sauti ya wengi ni sauti ya Mungu,” alisema
Machali.
Katika mazungumzo yake, Machali
alimshutumu pia Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe na Mbunge wa
Kasulu Vijijini, Zaituni Buyogela (NCCR-Mageuzi), kwamba wanachangia kukiharibu
chama hicho wilayani Kasulu.
“Viongozi wa Jimbo la Kasulu
Vijijini hawawezi kunifanya mimi na wana NCCR-Mageuzi Kasulu Mjini kuwa watumwa
wa fikra zao mgando kwa sababu nilikwenda darasani kusoma ili nielimike na
elimu yangu niitumie kwa manufaa na maendeleo ya jamii yangu.
“Ukweli unauma na wakati mwingine
unatuponza wachache, kwa hiyo, sitaogopa kusema ukweli na kutetea
ninachokiamini hata kama nawaudhi baadhi ya wenzagu,” alisema.
Pia aliwataka polisi wilayani Kasulu
wasiwakamate ovyo waendesha bodaboda kwa kuwa bodaboda zimekuwa msaada mkubwa
katika jamii.
Mwenyekiti wa NCCR –Mageuzi, Jimbo
la Kasulu Mjini, Benedickt Rukubigwa, alisema viongozi mzigo wa jamii ya
Mkemwema, wanatakiwa kuvuliwa madaraka kwa kuwa wanakiharibu chama chao.
“Mke Mwema ni bora akaombe uongozi
CCM ambako kuna watu wa aina yake kuliko kuendelea kukigawa na kukivuruga chama
chetu,” alisema Rukubigwa.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment