MAC PRODUCTION STUDIO'S

MAC PRODUCTION STUDIO'S
KWA MATANGAZO YA BIASHARA REDIONI( 0767-814844)

Wednesday 4 March 2015

PICHA NA TAARIFA YA MAZISHI YA KAPTEN JOHN KOMBA, RAIS AONGOZA MAMIA KUMZIKA KIJIJINI LUTUHI

Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Mbinga Mhashamu John Ndimbo akiongoza ibada ya mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi marehemu Kapteni John Damian Komba kijijini kwake Lituhi wilayani Nyasa Mkoani Ruvuma jana.(picha na Freddy Maro).
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiweka udongo katika kaburi la aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi marehemu Kapteni John Damian Komba
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumanne, Machi 3, 2015, ameungana na mamia ya waombolezaji kumzika Mbunge wa Jimbo la Nyasa na msanii mahiri wa muziki nchini, Mheshimiwa Kepteni John Damiano Komba, kwenye makaburi ya Kanisa Katoliki katika Kijiji cha Lituhi, Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma.

Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Songea,..........
akitokea Dar es Salaam, kiasi cha saa tano na robo asubuhi, Rais Kikwete amekwenda moja kwa moja Lituhi, karibu kiasi cha kilomita 140 kutoka mjini Songea, kwa ajili ya mazishi ya Mheshimiwa Komba ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Rais Kikwete amejiunga na waombolezaji akiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda kiasi cha saa tisa mchana kwa ajili ya mazishi ya mmoja wa wasanii ambao walijijengea heshima kubwa kwa nyimbo zake za uhamasishaji.

Wakati wa shughuli za mazishi ambazo kidini zimeongozwa na Askofu John Ndimbo wa Jimbo Katoliki Mbinga, waombolezaji walisomewa salamu za rambirambi ambazo zimetumwa na Rais wa Pili wa Malawi, Mheshimiwa Bakili Muluzi ambaye sasa amestaafu.

Katika salamu hizo, Mheshimiwa Muluzi amesema: “Nilimjua Komba kama rafiki na taarifa za kifo chake cha ghafla zimenistua sana.”

Mwili wa Marehemu Komba uliteremshwa kaburini saa 9:30 mchana huku ukishuhudiwa na mjane wa marehemu Salome Komba na watoto wake 11.

Rais Kikwete ameondoka Lituhi mara baada ya mazishi kurejea mjini Songea kumalizia ziara yake ya siku mbili ya kikazi mkoani Ruvuma.
Ends
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
3 Machi, 2015

Na Mwanaharakati.

No comments: