MAC PRODUCTION STUDIO'S

MAC PRODUCTION STUDIO'S
KWA MATANGAZO YA BIASHARA REDIONI( 0767-814844)

Monday, 4 May 2015

SABABU YA RAIS KIKWETE KUTEUA KATIBU MPYA WIZARA MAMBO YA NJE KUTOKEA KAGERA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, amemteua Balozi Liberata Rutageruka Mulamula kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kwa sasa Balozi Mulamula ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico.

Rais Kikwete pia amemteua Balozi Hassan Simba Yahya kuwa naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo  ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.  Kwa sasa Balozi Yahya ni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati Wizarani hapo.

Uteuzi huu umeanza tarehe 2 Mei, 2015

Je Balozi Liberata ni nani?


Balozi Liberata Rutageruka Mulamula ni mwanadiplomasia mwaandamizi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mbali ya kuiwakilisha Tanzania katika balozi mbalimbali za nje, amewahi pia kuwa Mshauri wa Rais Jakaya Kikwete katika masuala ya diplomasia. Na mwisho  Mulamula alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico.
 Hii yaweza kuwa sababu kuu? 

"Sijioni katika nafasi yoyote ile ya kisiasa. Mimi ni mtendaji, nipo kwa ajili ya kuwatumikia wanasiasa. Mpaka dakika hii, sina kabisa matamanio ya kuingia katika siasa. Akijitokeza mwanamke 2015, nitakuwa tayari kumuunga mkono ilimradi tu awe mwanamke mwenye sifa za uongozi, si bora mwanamke. Wanawake tukiamua kushikamana, tukiamua kujipanga, tunaweza kumpata Rais mwanamke".( Alissema hayo baada ya kuhojiwa na gazeti la raia mwema nchini tanzania September 2013)  

Balozi Mulamula katika mahojiano hayo, alizungumzia ukaribu wake?Tanzania na Marekani kupitia rasi Obama: "Kwa kweli naweza kusema nilipewa nafasi ya kwanza na ya kipekee. Siku niliyopeleka hati zangu za utambulisho kulikuwa na mabalozi wenzangu wengine kutoka mataifa mbalimbali. Niliwasilisha utambulisho wangu siku tatu tu baada ya kuripoti, kitu ambacho si cha kawaida kwa Marekani mtu kupata mihadi ya kuonana na Rais wa Marekani ndani ya siku tatu tu, baada ya kuripoti ofisini. Lakini kwangu iliwezekana.


Lakini pia, kama ninavyosema siku hiyo kulikuwa na mabalozi wengine, kwa hiyo ratiba yangu ilifanywa mwisho, nadhani alitaka tupate fursa na muda mrefu wa kuzungumza naye bila kuwapa bughudha wageni wengine. Zamu yangu ilipofika, Obama mwenyewe aliinuka kutoka kwenye kiti chake na kuja kunisubiri mlangoni kwake. Aliponiona tu alinikumbatia na kuniambia nawapenda sana Watanzania, naipenda Tanzania, karibu sana. Akasema sisi Wamerekani tunataka kufanya kazi na ndugu zetu Watanzania.

Unajua nilikwenda ofisini kwake wakati ambao Obama alikuwa bado anakumbuka ziara yake ya Tanzania na jinsi Watanzania tulivyompa mapokezi makubwa. Akasema ziara yake Tanzania ilikuwa juu, hajawahi kupata mapokezi mahali pengine popote katika nchi yoyote kama aliyoyapata Tanzania. Kwa kweli jina la Tanzania kwa Serikali ya Marekani na Wamarekani liko juu mno. 

Katika mazungumzo yetu hayo, akaniambia nimwambie Rais Jakaya Kikwete, anamshukuru sana kwa mapokezi aliyompatia. Akanihakikishia kwamba yote ambayo serikali yake iliahidi kwa Tanzania wakati wa ziara yake, itayatimiza, akanitaka nishirikiane naye kuhakikisha yote anayafanikisha.

Kama unakumbuka aliahidi umeme kwa Afrika na Tanzania ikawekwa katika nchi za mwanzo zitakazofaidika na mradi huo wa nishati ya umeme. Akasema atafanya kila jitihada kuwahamasisha wafanyabiashara wa Marekani kuja kuwekeza Tanzania na kuwajengea uwezo vijana wa Afrika katika masuala ya uongozi. Lakini aliahidi kuisaidia nchi yetu katika mapambano dhidi ya ujangili na utoroshaji wanyamapori".
 

Na Mwanaharakati.

No comments: