.
Atengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu TPA
.
Amsimamisha kazi Katibu Mkuu Uchukuzi
.
Waziri Mkuu awasimamisha kazi watumishi wengine 13 wa bandari
RAIS Dkt. John Pombe Magufuli
amevunja Bodi ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa
Bodi ya Bandari, Prof. Joseph Msambichaka pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari,
Bw. Awadhi Massawe.
Dkt. Magufuli pia ametengua uteuzi
wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Shaban Mwinjaka kuanzia leo
(Jumatatu, Desemba 7, 2015), na kwamba atapangiwa kazi nyingine.
Akitangaza uamuzi huo mbele ya
waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika leo ofisini kwake Magogoni,
jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hatua hizo
zimechukuliwa kufuatia ziara mbili za kushtukiza alizozifanya katika mamlaka ya
bandari Novemba 27 na Desemba 3, mwaka huu.
Waziri Mkuu amesema Rais Magufuli
amevunja bodi hiyo na kutengua uteuzi wa viongozi hao kutokana na utendaji
mbovu wa muda mrefu wa Mamlaka ya Bandari na kwa kitendo cha viongozi hao
kutochukua hatua kwenye vyanzo.
Pia alisema Katibu Mkuu
amesimamishwa kazi kwa sababu ya kutosimamia kwa makini mashirika mawili ya
Bandari na Reli ambayo yako chini ya wizara yake ambako yeye mwenyewe alizuru
Shirika la Reli (TRL) Desemba 3, 2015 na kukuta kuna ubadhirifu wa sh. bilioni
16.5/-.
“Tarehe 3 Desemba mwaka huu
nilifanya ziara ya kushtukiza pale TRL nikakuta wametumia visivyo sh. bilioni
13.5/- walizopewa na Serikali. Pia nilikuta wamekopa sh. bilioni 3/- kutoka
benki ya TIB lakini nazo wamezitumia nje ya utaratibu. Fedha hizi zilikuwa ni
za kusaidia kuboresha miradi ya shirika lakini wao wamezitumia visivyo.
Uchunguzi bado unaendelea,” alisema Waziri Mkuu.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi kuanzia leo
viongozi watano wa sekta zilizotoa ruhusa ya makontena kutoka ndani ya bandari
pamoja na watumishi wanane wa bandari kavu ambao walihusika na ukwepaji kwa
makontena 2,387.
“Viongozi hawa hawakuwemo kwenye
ripoti ya ukaguzi lakini ni wahusika wakuu. Hawa ndiyo waliotoa ruhusa ili
makontena yaende kwenye ICDs. Nao ni aliyekuwa Meneja Mapato ambaye kwa sasa
amehamishiwa Makao Makuu kitengo cha Fedha, Bw. Shaban Mngazija;
aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Mkuu wa Bandari Kavu (ICD) – ambaye
amehamishiwa Makao Makuu kwa Naibu Mkurugenzi Co-operate Services, Bw. Rajab
Mdoe; Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Bw. Ibin Masoud; na Meneja Bandari Msaidizi –
Fedha, Bi. Apolonia Mosha
Pia amewasimamisha kazi wasimamizi
wanane wa Bandari Kavu (ICDs) ambao ni Happygod Naftari, Juma Zaar, Steven
Naftari Mtui, Titi Ligalwike, Lydia Prosper Kimaro, Mkango Alli, John Elisante
na James Kimwomwa ambaye alihamishiwa Mwanza lakini kuanzia sasa anasimamishwa
kazi huko huko aliko.
“Bila wao kuidhinisha hakuna kontena
linaweza kutoka au kwenda kokote. Watumishi wote hao wawe chini ya ulinzi na
waisaidie polisi kupata taarifa hayo makontena ni ya nani na yana thamani
gani,” Waziri Mkuu alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa aliwaeleza
waandishi wa habari kwamba Desemba 3, mwaka huu aliamua kurudi tena bandarini
kufuatilia na kuangalia hatua ya udhibiti wa upitishaji wa bidhaa mbalimbali
kinyume cha utaratibu. “Ziara yangu ilinipitisha hatua zote za upitishaji
mizigo ambazo pia kwa mujibu wa Taarifa ya Ukaguzi wa Ndani ya tarehe 30 Julai
2015, Mamlaka ya Bandari iligundulika kuwepo kwa mianya mingi ya ukwepaji kodi
ikiwemo makotena 2,387 yaliyopitishwa kati ya Machi – Septemba 2014 kinyume cha
utaratibu”.
“Vitendo hivi vinaonyesha kuwa
bandari yetu hupitisha makontena mengi bila ya kulipiwa kodi na hakuna hatua
yoyote inayochukuliwa. Serikali haitavumilia kuona watu wachache au kikundi
chochote kilichojipanga kuhujumu mifumo au kuiibia Serikali kwa namna yoyote
ile kwa manufaa ya wachache kwani bandari ni eneo muhimu ambalo likisimamiwa
vizuri, linaweza kukusanya fedha nyingi na kuchangia Pato la Taifa,” alisema.
Desemba 3, mwaka huu, Waziri Mkuu
alimpa saa tatu tu Kaimu Meneja wa Bandari, Bw. Hebel Mhanga amletee ofisini
majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi huo. Pia alimpa Meneja
huyo wiki moja kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo
kutoka kwenye billing system na badala yake kuweka mfumo wa malipo wa
kielektroniki (e-payment). Mwisho wa kukamilisha zoezi hilo ni Desemba 11,
2015.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment