WADADISI wa Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi
Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18 wameaswa kuzingatia maadili ya kazi wakati wa
zoezi la kuorozesha kaya linalotarajia kuanza kesho ikiwa ni sehemu ya
maandalizi ya utafiti huo.
Akizungumza
wakati wa mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa wadadisi
hao, Meneja wa Takwimu za Jamii na Watu, Sylvia Meku kutoka Ofisi ya Taifa ya
Takwimu amesema ili kufanikisha zoezi la uorodheshaji wa kaya, ni lazima
wadadisi hao wakazingatia maadili ya kazi pamoja na kufuata taratibu zote za
Utumishi wa Umma.
“Ofisi
ya Taifa ya Takwimu inawaagiza kwenda kwenye jamii kwa ajili ya kuorodhesha
kaya zitakazofanyiwa Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania
Bara wa Mwaka 2017/18. Natumaini mtatii na kuheshimu maadili ya Utumishi wa
Umma ili muweze kufanikisha kazi hii kwa ufanisi,” amesema Slyvia Meku.
Amesema Uorodheshaji wa Kaya litafanyika mikoa yote ya Tanzania Bara kwa
takribani siku 15 kuanzia kesho Julai 11, 2017 na baadae kufuatiwa na utafiti
wenyewe unaotarajia kuanza mwezi Desemba, 2017.
Sylvia Meku amesema utafiti huu unafanywa na Ofisi ya Taifa
ya Takwimu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na baadhi ya Wadau wa
Maendeleo kwa lengo la kuangalia kiwango cha umasikini nchini.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment