Washington
DC;Mhe. Benjamin
William Mkapa, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewaasa
viongozi wa Nchi za Kiafrika kuchukua hatua ya kuhamasisha jamii za kiafrika
kuhusu mpango wa tohara ya hiari kwa wanaume (Voluntary Medical Male
Circumcision for HIV Prevention) kama mojawapo ya njia ya kupunguza maambukizi
ya UKIMWI barani Afrika.
Mheshimiwa
Mkapa aliyasema hayo alipokuwa anahitimisha mojawapo ya mijadala ya pembeni
(Satelite Session) iliyokuwa inaendelea wakati wa
Kongamano la XIX la Kimataifa la UKIMWI linaloendelea Mjini Washington DC,
Marekani ambapo watu takribani 22,000 wanahudhuria. Mjadala huo uliovutia mamia
ya wajumbe hususan kutoka Afrika kuhusu tohara ya hiari kwa wanaume,
uliendeshwa na Bi. Brenda Wilson kutoka Afrika Kusini ulielezea tafiti za
kisayansi kuhusu mpango huo kama njia ya kupunguza maambukizi ya UKIMWI.
Rais
Mkapa alisema mpango huu ni muhimu kutekelezwa na viongozi wa nchi za Kiafrika
kwani imethibitishwa na tafiti zilizofanyika kwa Waafrika kwamba unapunguza
maambukizi kwa asilimia 60, ambapo alisema si jambo dogo katika harakati za
kutokomeza UKIMWI. Aliongeza kuwa ni mpango uliopendekezwa na sisi Waafrika wenyewe
na ni wa hiari na hivyo hakuna atakayeshurutishwa.
“Umebuniwa
na nchi za magharibi, lakini umetafitiwa na kuthibishwa na sisi Waafrika
wenyewe, hivyo ni mpango wetu huu” alisisitiza Rais Mkapa huku akishangiliwa
kwa makofi na wajumbe wa mjadala huo.
Ili
kutekeleza mpango huu wa tohara ya hiari kwa mafanikio, Mhe. Mkapa alielekeza
mambo matatu. Kwanza nchi za kiafrika inabidi zitengeneze sera na mikakati
madhubuti ya jinsi ya kukabiliana na janga hili la UKIMWI. Pili mipango na
mikakati hiyo imilikiwe na wananchi wa nchi husika ili wao wenyewe wathibitishe
ushiriki wao na sio kuonekana kama shuruti .Na mwisho mipango na sera za
kukabiliana na UKIMWI itekelezwe kwenye mazingira ya ukweli na uwazi ili jamii
za kiafrika ziweze kutambua athari za janga hili la UKIMWI. Pia serikali nazo
zitenge fedha za kusaidia katika mapambano haya na si kutegemea fedha za
wafadhili tu.
“Umefika
wakati sasa dunia nzima ielekeze nguvu zake kwenye kutokomeza ugonjwa huu
hatari ambao unaua maelfu ya watu kila siku” Alisema Mhe. Mkapa na kuongeza
kuwa mataifa mbalimbali duniani hutoa misaada haraka sana mara majanga ya
dharura yanapotokea, kama vile mafuriko, ajali n.k. Lakini janga la
UKIMWI ni kama dharura inayoendelea na sasa ni wakati muafaka dunia nzima
itazame janga la UKIMWI kama dharura na inayoendelea.
Naye
Mwenyekiti mwenza wa Mpango wa Tohara ya Hiari wa PEPFAR Dkt. Emmanuel
Njeuhmeli alithibitisha tafiti hizo kwa kutoa mfano wa Zimbabwe ambapo
maambukizi ya UKIMWI yanakadiriwa kupungua kwa asilimia 45 ndani ya kipindi cha
miaka mitano ya utekelezaji wa mpango huo.
Wengine
walioongea katika mjadala huo ni Angelo Kaggwa (Uganda), Mhe. Dkt. Speciosa
Wandira (Uganda), Bi. Henrica Okondo (Kenya), Chifu Jonathan Mumena (Zambia),
Mhe. Oburu Oginga (Kenya), Mhe. Dkt. Christine Ondoa (Uganda), na Mhe. Blessing
Chebundo (Zimbabwe). Mjadala huo pia ulihudhuriwa na marais wastaafu
wanaojishughulisha na mapambano dhidi ya Ukimwi ( wajulikanao kama
Champions for AIDS Free Generation)Mhe. Joachim Chisano, Rais Mstaafu wa Msumbiji
na Mhe. Kenneth Kaunda, Rais Mstaafu wa Zambia
Mhe.
Mkapa amehudhuria Kongamano hili kubwa la UKIMWI kwa mwaliko wa taasisi ya
Champions for HIV-Free Generation inayoongozwa na Rais Mstaafu wa Botswana Mhe.
Festus Moghae, ambapo Mhe. Mkapa ni mmoja wa Ma-Champion nane wa taasisi hiyo.
Kongamano
la XIX la Kimataifa la UKIMWI limeanza Washington DC tarehe 22 Julai hadi 28
Julai 2012 ambapo watu mashuhuri na viongozi mbalimbali wa Marekani
wamehudhuria akiwemo Rais wa Marekani Mhe. Barack Obama.
Imetolewa
na Ubalozi wa Tanzania Marekani
Julai
25, 2012
No comments:
Post a Comment