MAC PRODUCTION STUDIO'S

MAC PRODUCTION STUDIO'S
KWA MATANGAZO YA BIASHARA REDIONI( 0767-814844)

Wednesday 27 February 2013

TANZANIA YAPATA MFUMO WA UTAMBUZI WA BIDHAA


TATIZO la Tanzania la kuuza bidhaa nje na kushindana katika Soko la Kimataifa limetatuka baada ya sasa kuwa imeingia katika mfumo wa kimataifa wa utambuzi wa bidhaa kwa kutumia Nembo za Mistari (Bar Code).
Hayo yalifahamika wakati  Waziri Mkuu Mizengo Pinda  anazindua mpango mkakati wa miaka mitano wa taasisi inayosimamia nembo hiyo nchini Global Standard One (GS1) – Tanzania National Ltd., kwenye ukumbi wa Blue Pearl Hotel, Ubungo jijini Dar es Salaam leo (Jumatano Feb. 27, 2013) mchana.
Namba ya utambulisho ya nembo hiyo kwa Tanzania ni 620 na tayari imeunganishwa katika mtandao wa GS1 duniani. Mpaka sasa wazalishaji 370 wa bidhaa mbalimbali wamekwishapata na wanatumia nembo hiyo wakiwa na jumla ya bidhaa 6,000 sokoni.
“Hili ni jambo jema. Bado nina imani kwamba tunaweza kufanya vizuri zaidi  na kupiga hatua kubwa zaidi kama tukidhamiria. Changamoto ninayoiona sasa ni jinsi ya kutangaza mafanikio hayo ambayo tayari tumeyafikia,” Pinda alisema.
Waziri Mkuu aliitaka GS1 Tanzania, kutumia matangazo ya Televisheni, kushiriki katika Maonyesho ya Kilimo na Nane Nane na Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara kutangaza nembo hiyo ili wazalishaji wengi zaidi wajiungenayo.
GS1 ni Shirika la Kimataifa lisilo la kiserikali na lisilo la faida lililoanzishwa mwaka 2005 na lenye makao makuu yake Brussels, Ubelgiji. Shirika hilo limeisaidia Tanzania kuanzisha shughuli hiyo nchini, miaka miwili iliyopita.
Kabla ya GS1 Tanzania, wazalishaji wa bidhaa wa Tanzania walikuwa wanapata nembo Kenya na Afrika Kusini na kuonyesha kama vile bidhaa hizo zinatoka katika nchi hizo.
Waziri Mkuu alisema kuanzishwa kwa GS1 Tanzania ni sehemu ya matokeo ya nia ya serikali ya awamu ya nne kuhakikisha kuwa chombo hicho kinaanzishwa nchini kama moja ya taasisi za viwango nchini.
Alisema nembo hiyo ni fursa nzuri kwa wazalishaji, hasa wajasiriamali wadogo, kupenya kwenye soko la kimataifa na kupata biashara nzuri na fedha nyingi.
Pinda aliliagiza Shirika la Viwango nchini TBS na Wakala wa Usajili wa Makampuni na Leseni za Biashara, kutoa umuhimu wa kwanza kwa wazalishaji wadogo wanapotaka kupatiwa nembo ya viwango na kusajili biashara.
“TBS muwe na kitengo cha wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali. Msiwachanganye hawa na wafanya biashara wakubwa, mtawabana sana na watashindwa kunyanyuka,” alisema.
Katika sherehe hiyo, Waziri Mkuu alizindua mpango huo kwa kukata utepe na kuanzisha king’ora. Pia litoa mfano wa nembo hiyo ya mistari kwa wazalishaji mbalimbali.
Waziri Mkuu pia yeye mwenyewe alikabidhiwa nembo hiyo kwa kuzalisha asali.
(mwisho)
Imetolewa na:
          Ofisi ya Waziri Mkuu,
          S.L.P. 3021,
          DAR ES SALAAM

No comments: