Wizara ya
Kazi na Ajira imekua ikipokea malalamiko toka kwa wadau mbalimbali kuhusu
utaratibu wa udalali wa kukodisha wafanyakazi katika makampuni unaofanywa na
baadhi ya Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira nchini.
Wizara
imefanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hili na kubaini kuwa utaratibu wa
kukodisha wafanyakazi unaofanywa na baadhi ya Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira
ni kinyume cha Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya Mwaka 1999 [Sura
243 kama ilivyorejewa Mwaka 2002]. Kwa mujibu wa Kifungu 4 cha
Sheria hii, majukumu ya msingi ya Wakala wa Huduma za Ajira ni kuwaandaa na
kuwaunganisha Watafuta Kazi na Waajiri kwa kutoa mafunzo na ushauri
elekezi kwa watafuta kazi, kutafuta fursa za ajira na kutoa taarifa za
soko la ajira. Hivyo, Mawakala hawapaswi kuwa waajiri wa wafanyakazi
waliowatafutia kazi kwa niaba ya Waajiri wengine.
Aidha,
uchunguzi umebaini kwamba utaratibu huu ni ujanja unaotumiwa na baadhi ya
Waajiri na Mawakala kwa lengo la kukwepa kodi na kujipatia faida kwa kukwepa
kutoa haki za msingi za wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria za Kazi. Baadhi ya
makampuni yanayokodisha wafanyakazi yamefanyiwa uhakiki na TRA na kubainika
kukwepa kodi ya mapato ya ajira (PAYE) na na kodi ya mapato ya kampuni
kinyume na Kifungu cha 7 cha Sheria ya Kodi ya Mapato ya Mwaka 2004
[Sura 332 kama ilivyorejewa Mwaka 2008].
4.Uchunguzi
huu umebaini athari mbalimbali kwa wafanyakazi wanaoajiriwa kwa utaratibu
huu. Athari hizo ni pamoja na:
-Wafanyakazi
kukosa haki ya hifadhi ya jamii kama vile likizo ya uzazi na matibabu
kinyume na Sheria mbalimbali za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii;
-Uwepo wa
ubaguzi katika malipo ya mishahara kwa kazi ya aina moja kinyume na
kifungu cha 7(10) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya mwaka 2004
ambacho kinamtaka mwajiri kuchukua hatua stahiki kwa kuhakikisha kuwa
wafanyakazi bila kujali jinsia zao wanalipwa mishahara linganifu na ya haki kwa
kazi yenye uzito na thamani sawa;
-Kukosa
fursa za kujiendeleza kielimu na mafunzo;
-Kukosekana
kwa usalama na uhakika wa ajira ;
-Wafanyakazi
kulipwa mishahara ya kima cha chini kinyume na sekta wanayofanyia kazi.
Kwa taarifa
hii, Wizara ya Kazi na Ajira imeamua kusitisha mara moja utaratibu wa Mawakala
kuwaajiri wafanyakazi wanaowatafutia kazi. Aidha, Mawakala
na Kampuni husika waliopo katika utaratibu huu kwa sasa wanapaswa
kuwahamisha wafanyakazi waliokodishwa kutoka kwa Wakala kwenda kwa
Kampuni husika. Waajiri na Wakala wanatakiwa kukamilisha zoezi hili ndani ya
kipindi cha mwezi mmoja na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa Katibu Mkuu,
Wizara ya Kazi na Ajira kabla au ifikapo tarehe 28/02/2014.
Uchunguzi
zaidi unaendelea kubaini kama kuna wafanyakazi wa Kigeni wanaohusishwa katika
utaratibu wa kukodishwa ili hatua zinazotahili ziweze kuchukuliwa ikiwa ni
pamoja na kuwataka waombe vibali vya ajira kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji
Na.7 ya mwaka 1995 na Sheria ya Huduma za Ajira Na.9 ya mwaka 1999. Wageni
watakao kidhi vigezo wataajiriwa na kampuni walipokodishwa; ambazo kwa wakati
huo zitakua ndiyo mwajiri wao.
Wizara ya
Kazi na Ajira inawaelekeza Wakala wa Huduma za Ajira nchini kwamba, kwa
utaratibu wa sasa watapaswa kuwasilisha barua za maombi ya usajili wa
Uwakala kwa KAMISHNA WA KAZI kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za
Ajira Na. 9 ya mwaka 1999 [Sura 243 kama ilivyorejewa Mwaka 2002]
ili waweze kufanya shughuli za Uwakala wa Huduma za Ajira kisheria. Maombi haya
yawasilishwe ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu kutolewa kwa tangazo hili.
Baada ya muda huo Wakala asiye na kibali cha Kamishna wa Kazi hatoruhusiwa
kuendesha shuguli za huduma za ajira nchini. Aidha, Mawakala watakaopata leseni
ya Kamishna wa Kazi yatakua yakitangazwa ili yatambuliwe na Umma.
Nasisitiza,
maelekezo haya yatatolewa kwa Makampuni na Wakala waliohusishwa katika
uchunguzi kwa ajili ya utekelezaji.
MWANA HARAKATI
No comments:
Post a Comment