Mmoja
wa vigogo hao anayefanya kazi katika wizara nyeti, ametajwa 'kumpigania'
bilionea aliyekamatwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam akituhumiwa kuhusika
na shehena ya kilo 210 za dawa za kulevya aina ya heroin zinazokisiwa kuwa na
thamani ya Sh bilioni 10 ambazo zilikamatwa nchini mwaka 2012 mkoani Lindi.
Tayari bilionea
huyo, Ali Khatib Haji 'Shikuba' ameshafunguliwa mashitaka, kesi yake
ikiunguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Lindi.
Kwa mara ya kwanza
alipandishwa kizimbani Machi 13 mwaka huu akiunganishwa na watuhumiwa wengine,
Maureen Liyumba, Othman Mohammed Nyamvi au maarufu kwa jina la Ismail Adam na
Upendo Mohammed Cheusi ambaye kwa sasa ni marehemu.
Kwa mara ya pili
wanatarajiwa kupandishwa kizimbani kesho mbele ya Kaimu Hakimu Mfawidhi wa
Mahakama ya Mkoa wa Lindi, Allu Nzowa.
Habari za uhakika
ambazo mwandishi amezipata zinasema tangu kukamatwa kwa Shikuba, kigogo huyo
amekuwa akihaha kutaka kumnusuru mfanyabiashara huyo maarufu dhidi ya kesi
inayomkabili.
Kukamatwa kwa
Shikuba kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Kudhibiti Dawa za
Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa.
"Ni kweli
tumemkamata. Juhudi zetu zimefanikiwa kukamata mmoja wa watu wazito
wanaohusishwa na biashara hii," alisema.
Ingawa `mzigo'
anaohusishwa nao Shikuba ulikamatwa mwaka 2012, inaelezwa hakukamatwa kutokana
na mfanyabiashara huyo kuwa mafichoni nchini Afrika Kusini na kwamba akiwa
huko, alitumia hila na kupata hati nyingine ya kusafiria iliyotolewa Februari
28, mwaka huu, hivyo kurejea nchini alikokumbana na vijana wa Nzowa mara baada
ya kutua kwa ndege ya shirika la Ndege la Afrika Kusini, South African Airways.
Mara baada ya
kumkamatwa, alisafirishwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi hadi mkoani
Lindi.
Katika miaka ya
hivi karibuni, Serikali kupitia kikosi cha kudhibiti dawa za kulevya kimekuwa
kikifanya jitihada kubwa za kupambana na wahusika wa dawa za kulevya, ikinasa
wengi katika maeneo mbalimbali, kuanzia viwanja vya ndege, hadi kwenye vyombo
vya usafiri wa majini, mfano ukiwa ni shehena iliyokamatwa Lindi na pia
nyingine ya heroine yenye uzito wa kilo 280 iliyokamatwa hivi karibuni katika
bahari ya Hindi, kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Na Mwanaharakati.

No comments:
Post a Comment