Wanafunzi wawili wa Shule ya
Sekondari ya Kibara, wilayani Bunda mkoani Mara wamefikishwa mbele ya Mahakama
ya Hakimu Mkazi wa Bunda wakikabiliwa na shtaka la kumshambulia na kumjeruhi
kwa panga mwalimu mkuu wa shule hiyo.
Ilielezwa kuwa wanafunzi hao walimjeruhi mwalimu huyo baada ya kutaka kurejeshewa fedha zao za ada kwa vile hawakuwa na mpango tena wa kuendelea na masomo shuleni hapo.
Hata hivyo imeelezwa kuwa uongozi wa shule hiyo ulipinga azma hiyo ya wanafunzi kuacha shule na kurejeshewa fedha zao.
Mwendesha Mashtaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Masoud Mohamed aliwataja washtakiwa hao wanaosoma kidato cha tatu kuwa ni Amosi Shirima (22) na James Athuman (22).
Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa
kutenda kosa hilo Machi 17 mwaka huu.
Mohamed alidai kuwa siku ya tukio, saa 5:00 asubuhi, washtakiwa hao kwa pamoja walimvamia mkuu wa shule, aliyetajwa kwa jina la Awadh Said wakati akiwa ofisini kwake shuleni hapo.
Baada ya kuvamia ofisini kwake,
watuhumiwa walimshambulia sehemu mbalimbali za mwili kwa panga na kusababisha
majeraha makubwa.
Masoud alisema baada ya mwalimu kuona anashambuliwa, alipiga kelele za kuomba msaada kabla ya watu kujitokeza na kuwakamata watuhumiwa na baadaye kuwapeleka kituo cha polisi.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa hali
ya mwalimu huyo siyo nzuri na anaendelea kupata matibabu hospitalini
alikolazwa.
Washtakiwa kwa pamoja wamekana shtaka lao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Safina Semfukwe.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment