Katika
kukabiliana na kasi ya maendeleo ya ukuaji wa uwekezaji katika maeneo ya
viwanda vikubwa na biashara za huduma mkoani Mtwara, Serikali imesema kuwa kuna
haja ya kuuimarisha Uwanja wa Ndege wa Mtwara ili kuongeza ufanisi katika
utoaji wa huduma kwa watumiaji wa uwanja huo, hasa kufuatia kugundulika kwa
gesi mkoani humo,
Hayo yamebainishwa mmoja wa viongozi
wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati ilipofanya ziara kwa ajili ya
kujionea maendeleo ya uwanja wa huo.
Bibi Mwanri alisema kuwa Serikali
inaendelea kufanya tathmini na mikakati mbalimbali itakayopelekea kuuimarisha
uwanja wa ndege wa Mtwara ili kuweza kuhudumia uwekezaji mkubwa unaofanywa na
makampuni mbali mbali ya ndani na nje ya nchi mkoani humo. Aliongeza:
“Tathmini ya awali inaonesha kuwa
miradi mingi ipo mkoani Mtwara kufuatia kugundulika kwa gesi hivyo kuna haja ya
dhati ya kuuimarisha uwanja wa ndege wa Mtwara kwa lengo la kutoa huduma za
uhakika wakati huu wa mfumuko wa kiuchumi mkoani Mtwara,” alisema Bibi Mwanri.
Akizungumza
wakati wa ukaguzi huo, Naibu Katibu Mtendaji (Uchumi Jumla), Prof. Longinus Rutasitara ambaye alikuwa kiongozi mwenza wa
ukaguzi, alisema kuwa kuna haja ya dhati ya kuwekeza katika uwanja huo ili
kukabiliana na kasi ya maendeleo ya mkoa wa Mtwara kufuatia wawekezaji wengi
kuendelea kumiminika na kuwekeza mkoani humo.
“Uwanja wa ndege wa Mtwara una fursa
za nyingi za kuhudumia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, hakika ni lango
la biashara hasa kipindi hiki cha uchumi wa gesi mkoani Mtwara, hivyo
uendelezaji wa uwanja huu ni jambo lisilo epukika,” alisema Prof. Rutasitara.
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16), Miundombinu ni kipaumbele cha
kwanza, hasa uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya nishati, usafirishaji
(bandari, reli, barabara na usafiri wa anga), maji (safi, taka na ya uzalishaji)
na TEHAMA.
Serikali imeandaa Mpango wa
Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 -2015/16) wa kutekeleza Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025. Lengo kuu la Mpango huu ni kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa
nchi ili kuweka misingi ya ukuaji mpana wa uchumi na unaolenga watu walio
masikini zaidi. Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano unawianisha
katika mfumo mmoja wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ili kutoa
mwongozo wa utekelezaji na kuipa Serikali fursa na mfumo rasmi wa ufuatiliaji
na tathmini wa miradi ya maendeleo kitaifa.
Picha na Saidi Mkabakuli
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment