MAC PRODUCTION STUDIO'S

MAC PRODUCTION STUDIO'S
KWA MATANGAZO YA BIASHARA REDIONI( 0767-814844)

Tuesday, 18 March 2014

RIPOT YA MV KILIMANJARO IMEKABIDHIWA, UNDANI UKO HAPA

Ni baada ya kufanyiwa kazi na tume ya watu watano.

Mwenyekiti wa Bodi ya kuchunguza ajali ya Meli ya MV. Kilimanjaro 2, Khamis Ramadhan Abdallah (kushoto) akikabidhi Ripoti ya Bodi hiyo baada ya kukamilika kwa Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano Rashid Seif Suleiman Ofisini kwake Kisauni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Bodi ya kuchunguza ajali ya Meli ya MV. Kilimanjaro 2 leo imekabidhi rasmi Ripoti ya ajali hiyo baada ya kumaliza kazi hiyo kwa Waziri wa  Miundo mbinu na Mawasiliano Rashid Seif Suleiman Ofisini kwake Kisauni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Akikabidhi Ripoti hiyo Mwenyekiti wa Bodi hiyo Khamis Ramadhan Abdallah amesema kazi hiyo waliyopewa wameweza kuimaliza kwa mujibu wa siku walizopewa na walikuwa huru bila ya kuingiliwa na mkono wa Serikali wala Taasisi yoyote.
Aidha alisema Bodi ilifanya kazi katika mazingira magumu lakini walichukulia kazi hiyo niyanyumbani na niwajibu wao kufanya kwa Maslahi ya wananchi wa Zanzibar.
Hata hivyo alisema hapo awali kazi hiyo walipangiwa kuifanya kwa kipindi cha mwezi mmoja lakini kutokana na uzito wa kazi hiyo na majukumu mengine walilazimika kuomba mwezi mmoja ambapo kazi hiyo walitakiwa kuikabidhi kesho na badala yake wameweza kuikabidhi leo.
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Rashid Seif Suleiman ameipongeza Bodi hiyo kwa kufanya kazi bila ya upendeleo na zaidi walizingatia uhalisia wa kazi yao na siyo kubabaishwa na Mtu.
Aidha alisema chombo hicho hakikuundwa kwa kutafutwa nani mbaya wala mkosa wa ajali hiyo bali kimeundwa kwa ajili ya kuangalia mapungufu yaliyopo na kuweza kurekebishwa ili Wazanzibari wasizidi kuumia.
Hata hivyo alisema dalili nzuri ipo katika Ripoti hiyo na kazi iliyobaki ni kuisoma kwa kina na kisha kukabidhi katika Mikono ya Serikali kuu kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Naibu Katibu mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Tahir A.K Abdullah amesema Wananchi hivi sasa wanasubiri kuona Serikali imefanya nini tokea ajali hiyo imetokea ambapo aliwatoa wasiwasi kuwa haki  itatendeka kwa mujibu wa uchunguzi uliofanyika.
Bodi hiyo ya Wajumbe watano iliyoundwa chini ya Sheria ya Usafiri wa Baharini kifungu no. 4552 na 4551 ya mwaka 2006 imeundwa kufuatia ajali ya Meli ya MV. Kilimanjaro 2 iliyotokea Miezi miwili iliyopita katika Mkondo wa Nungwi ilipokuwa ikitokea Pemba kuja Unguja.
Na Mwanaharakati.

No comments: