Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amechaguliwa kuwa Kiongozi Mwenye
Mchango Mkubwa zaidi katika Maendeleo Barani Afrika mwaka 2013 .
Heshima hiyo kwa Rais Kikwete
imetolewa na jarida maarufu la kimataifa la African Leadership Magazine Group
na Tuzo la heshima hiyo itatolewa jioni ya leo, Jumatano, Aprili 9, 2014,
katika sherehe iliyopangwa kufanyika Hoteli ya St. Regis mjini Washington, D.C
ikiwa ni pamoja na chakula cha jioni.
![]() |
| Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard katika ubalozi wa Tanzania nchini Marekani mjini Washington DC Marekani, na atapokea tuzo ya Africa’s Most Impactful Leader of the Year kwa niaba ya Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania mjini humo leo. PICHA NA IKULU. |
Tuzo hiyo ya heshima kubwa hutolewa
kwa viongozi wa Afrika ambao hutoa mchango mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii
kila mwaka kwa watu wao na limetolewa kwa Rais Kikwete kwa mafanikio makubwa
kwa masuala ya utawala bora.
Jarida hilo linasema kuwa ukweli wa
hali hiyo bora ya utawala bora, chini ya uongozi wa Rais Kikwete
umeendelea kumiminiwa sifa kimataifa na leo umeifanya Tanzania kuwa nchi ya
kuigwa mfano kama kituo cha uhakika cha uwezeshaji kutokana na mageuzi makubwa
yaliyofanywa katika sera na mifumo ya uchumi.
Jarida hilo linasema kuwa Rais
Kikwete alikuwa chaguo kubwa na la kwanza la wasomaji wa Jarida hilo ambao
walipiga kura kupitia njia mbali mbali za mawasiliano za jarida hilo. “Kuhusu maoni ya wasomaji wetu juu ya
kiongozi yupi wa Afrika ambaye ni hodari zaidi kwa maendeleo ya kiuchumi na
maendeleo, matokeo ya majibu ya swali hilo yamedhihirisha bila shaka yoyote
kuhusu nafasi ya Rais Kikwete katika uongozi wa nchi yake. Na ushahidi uko kila
mahali – ameweza kusimamia uchumi ambao umekuwa kwa wastani wa asili mia saba
kwa miaka yote ya uongozi wake.”
Sherehe za leo, miongoni mwa mambo
mengine, zitaliwezesha Jarida hilo kutangaza mafanikio ya Tanzania chini ya
uongozi wa Rais Kikwete kwa Jumuia ya Kimataifa, ikiwa ni pamoja na Jumuia ya
Kimataifa ya Kibiashara, wanadiplomasia na taasisi nyingine zenye ushawishi
mkubwa katika medani za kimataifa na zenye makao yake katika Jiji la Washington
na maeneo ya jirani.
Imetolewa na: Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,Ikulu,
Na Mwanaharakati.


No comments:
Post a Comment