Na Saidi
Mkabakuli
Tanzania,
kama zilivyo nchi nyingi duniani kwa miaka mingi imekuwa mfuasi wa dhana ya
usawa na haki ili kuwa msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ili
kutimiza matakwa ya demokrasia.
Hali hii
imeifanya Serikali kufanya jitihada nyingi za kuboresha dhana hii licha ya
changamoto nyingi zinazokinzana na juhudi hizi za serikali.
Serikali ya
Tanzania kwa kuendeleza ufuasi wake kwa demokrasia na hasa suala zima la
utawala bora, sio tu ilianzisha wizara maalum kwa ajili ya kusimamia utawala
bora pia ilijiunga na Mpango wa Kujipima kwa kutumia vigezo vya Utawala Bora
(APRM) kwa kuwasilisha rasmi maombi ya kujiunga na mpango huu tarehe 26 Mei,
2004 na kukubaliwa rasmi tarehe 8 Julai 2004, wakati wa Kikao cha Tano cha
Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika.
APRM ni
mpango wa hiari, uliobuniwa na viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika, kuziwezesha
nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, kujitathmini katika utendaji wa shughuli za
serikali na shughuli zao nyingine kwa ujumla. Aidha mpango huu unalenga kuzipa
nchi wanachama, fursa ya kujifunza kutokana na uzoefu na mafanikio ya nchi
zingine za Kiafrika, na hivyo kuziwezesha nchi husika kuiga sera na mbinu
muafaka zilizoleta mafanikio hayo kwa manufaa ya nchi zao. Kwa ujumla, ombi la
kufanyiwa tathmini linapofanywa, linaashiria nchi husika kukubali kufuata
misingi ya utawala bora katika uendeshaji wa siasa na shughuli za kiuchumi na
wakati huohuo, kukubali kufanyiwa tathmini na Viongozi Wenza wa nchi za
Kiafrika.
Hadi sasa nchi 34 kati ya 54 wanachama
wa Umoja wa Afrika zimejiunga na mpango wa APRM. Mpango huo unahusisha uhakiki
katika vipindi mbalimbali (periodic reviews) wa sera, kanuni na taratibu za
utendaji zilizozoeleka (practice) ili kubaini maendeleo yaliyopatikana katika
kutekeleza malengo yaliyokubaliwa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na utawala
wa pamoja wa kibiashara kama ilivyoainishwa kwenye Tamko la Demokrasia, Siasa,
Uchumi na Utawala wa Pamoja.
Chimbuko la
APRM ni Mpango Mpya wa Maendeleo ya Afrika (New Partnership for Africa’s Development-NEPAD), ambao unalenga kuliondoa
bara la Afrika kutoka kwenye lindi la umaskini, na kuleta maendeleo. NEPAD
imeunganisha mipango ya maendeleo iliyobuniwa chini ya Umoja wa Nchi Huru za
Afrika, (OAU), na kuainisha ukosekanaji wa utawala bora kama
mojawapo ya vikwazo dhidi ya maendeleo yanayolikabili bara la Afrika. Hivyo,
ili kukabiliana na kikwazo hiki, viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika (UA)
walitoa Tamko Kuhusu Demokrasia, Siasa, Uchumi na Uongozi Bora katika nyanja za
uchumi na mashirika ya kibiashara. Tamko hilo
pia linaainisha mkakati wa kufanikisha azma hii, kupitia demokrasia na utawala
bora.
Lengo la msingi
la APRM ni kuhimiza utumiaji wa sera, viwango na miendeno inayokubalika
kitaalamu ili kujenga utengamano wa kisiasa, ukuaji chanya wa uchumi, maendeleo
endelevu na kuharakisha ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda na hatimaye bara
zima.
Pia, APRM inatoa
fursa ya kuchangia katika kudumisha utengamano, kuleta maendeleo pamoja na
kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kikanda kwa njia ya kubadilishana uzoefu na
kuiga mifano bora ikiwa ni pamoja na kutambua udhaifu na kutathmini mahitaji ya
kuongeza uwezo wa serikali na nchi.
Kwa kutambua umuhimu wa utawala bora, Mipango na
mikakati mingi ya kimaendeleo na ile ya kupambana na umaskini imekuwa
ikijumuisha kipengele cha utawala bora kama
moja ya misingi ya kufikia malengo. Kwa mfano, moja ya misingi ya Dira ya Taifa
ya Maendeleo (TDV) 2025, kati ya misingi minne ya utekelezaji, unahimiza
uimarishaji wa utawala bora na uongozi wa haki na kisheria ikiwa ni pamoja na
jamii kukataa rushwa, kuimarisha mifumo ya uongozi na utawala ili kuweza
kufikia malengo makuu ya Dira hiyo.
Pia, Mkakati
wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA)
I&II, sifa na misingi yake ni pamoja na Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini
wa Mapato; Kuboresha maisha ya watu na Ustawi wa Jamii; na Utawala bora na
uwajibikaji.
Suala kuu la
msingi linalojitokeza katika kila Mkakati ni Utawala bora na uwajibikaji. Dhana
hii ni msingi madhubuti katika kutekeleza mikakati hii yenye mkondo wa kiuchumi
na mingine mingi inayotekelezwa na Serikali. Hivyo basi, umuhimu wa APRM katika
mustakabali wa ustawi wa jamii ni chanya, kwa kuwa nchi inapata faida ya kujitathmini
pale inapokosea. Hivi karibuni Katibu Mtendaji wa Mpango huu (APRM) nchini Tanzania, Bibi Rehema Twalib alitoa taarifa kuwa
Tanzania
ni moja ya nchi zinazofanya vizuri katika utawala bora Barani Afrika.
Akizungumzia
umuhimu wa APRM katika kufikia lengo la msingi la mikakati hii, Bibi Twalib
anasema kuwa ni muhimu kudumisha utengamano, ili kuleta maendeleo pamoja na
kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kikanda kama
njia ya kubadilishana uzoefu ili kuiga mifano mizuri kutoka nchi zilizopiga
hatua kiuchumi.
Kwa mujibu wa Bibi Twalib, Tanzania
imepata mafanikio katika maeneo ya Usimamizi wa Uchumi, Maendeleo ya
Uchumi-Jamii Demokrasia na Utawala Bora, Siasa, Uendeshaji wa Kampuni na
Masuala Mtambuka kama Afya.
Bibi Twalib
alisema kuwa Tanzania
kupitia APRM, imefanya tathmini yake katika maeneo hayo na kuwasilisha ripoti
yake mbele ya wakuu wa nchi wanachama na kujadiliwa. Akizungumzia mikakati
iliyopo katika kuhakikisha kuwa malengo ya APRM yanakuwa chachu ya kukuza
uchumi wa nchi na kuleta maendeleo kwa jamii ya Kitanzania.
Bibi Twalib
aliongeza kuwa APRM kupitia Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania
inaendelea kuendesha tathmini ya utendaji wake na vyombo vyake kwa uwazi,
ukweli na umakini, kulingana na vigezo vilivyowekwa kwenye Mpango wa Kujipima
kwa kutumia Vigezo vya Utawala Bora.
“Kwa kutambua umuhimu katika kuimarisha utawala bora, Sekretarieti inaendelea
kutekeleza Mpango kazi wa kitaifa wa kujitathmini katika masuala ya utawala
bora (African Peer Review Mechanism -
National Plan of Action, APRM-NPoA),” aliongeza Bibi Twalib.
Kwa mujibu
wa APRM-NpoA,
moja
kati ya manufaa ya ya utekelezaji wa Mpango huu ni kubaini mambo mazuri juu ya
utawala bora nchini Tanzania
hali inayoongezea imani (confidence) wawekezaji toka nje ya nchi na wabia wa maendeleo.
Hili moja ya mafanikio ya APRM, maana kwa mujibu wa takwimu kutoka Kituo cha
Uwekezaji Nchini (TIC) mpaka kufikia mwezi Desemba, 2013 kilifanikiwa kusajili
miradi 9,442.
Hatahivyo, suala
la kushirikisha wananchi ni suala lisiloepukika, ambapo, Bibi Twalib anahimiza
suala la nafasi ya wananchi katika Mchakato huu. Bibi Twalib anasema kuwa, kwa
kuwa APRM ina njema ya kupanua wigo wa demokrasia, na kuwapa wananchi kauli
katika maamuzi yanayohusu mustakabali ya nchi yao.
“APRM Tanzania
inategemea kuwa wananchi watatumia kikamilifu, nafasi inayotolewa ili kutoa
tathmini yao ya
kweli, kuhusu yale wanayoyaona kuwa ni mapungufu ya utendaji serikalini na
mapungufu ya utawala bora nchini kwa ujumla, ili kuiwezesha serikali nayo
kuyabaini mapungufu hayo na kuyachukulia hatua muafaka” anasihi Bibi Twalib.
Anaongeza kuwa ikiwa wananchi watatumia vyema fursa
hizi vizuri, ndipo malengo ya kuanzishwa kwa Mchakato huu yatakapotekelezwa na
kuwezesha kutimia malengo na misingi ya mikakati ya Serikali ya kuivusha Tanzania kutoka
dimbwi la umaskini.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment