MAC PRODUCTION STUDIO'S

MAC PRODUCTION STUDIO'S
KWA MATANGAZO YA BIASHARA REDIONI( 0767-814844)

Saturday, 12 April 2014

VIFO VYA WATU WATATU MKOANI KAGERA


Watu watatu akiwemo afisa kilimo na mifugo wa kata, mwenyekiti wa kijiji na mwanakijiji mmoja, wameuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya kupigiwa yowe kuwa wezi wa mifugo.
Rpc Kagera George Mayunga
Tukio hilo limetokea majira ya saa sita za usiku wa kuamkia 12 april 2014 katika kijiji cha Kalongo kata ya Rwabwele wilayani Kyerwa  mkoani kagera.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Kyerwa ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo BENEDCT KITENGA, amesema kuwa mauaji hayo yamefuatia msako wa wizi wa mifugo uliofanywa na viongozi wa kijiji cha Kitale ili kubaini mifugo iliyokuwa imeibiwa katika kijiji hicho kwa muda wa wiki moja iliyopita.
Dc Kyerwa Benedict Kulikila Kitenga
Kwa mujibu wa  KITENGA viongozi hao walifika katika kijiji cha Kalongo wakitokea kijiji cha Kitale na kuwakuta ng’ombe waliokuwa wakiwatafuta baada ya kuibiwa katika kijiji hicho, kwa bwana Joas Augustino mkazi wa kijiji cha Kalongo.

Baada ya kuwakuta ng’ombe hao 12, waliamuru kuondoka na mtuhumiwa wa wizi wa ng’ombe hao bw.Augustino, ili kumfikisha katika mikono ya sheria kwa mujibu wa taratibu na kanuni za nchi.

Hata hivyo inadaiwa kuwa baada ya kuondoka na mtuhumiwa huyo nyumbani kwake mke wa mtuhumiwa alipiga yowe kuwajulisha wanakijiji cha Kalongo kuwa mmewe ametekwa na kuchukuliwa na majambazi.

Kufuatia yowe hilo lililo ambatana na ngoma ya kuashiria hatari, wanakijiji katika kijiji cha Kalongo walibeba silahaa mbalimbali ikiwemo mapanga na kuwanyatia viongozi hao waliokutwa wakiendelea na safari na kuwashambuliwa.

Katika maelezo ya baadhi ya wanakijiji hao wanadai kuwa, askari mgambo baada ya kuona kundi lao wanazidiwa nguvu, alikimbia kwa kujivuta vuta kutokana na madai kuwa alikatwa mguu ambao umesalia katika eneo la tukio, na mpaka sasa bado hafahamiki aliko.

Akizungumza tukio hilo   kamanda wa polisi mkoa Kagera Gorge Mayunga amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo, na kuwataja waliouwa kuwa ni Shimbwilo Jonathan (44) Juma Mbogo (48) na  Jacknus Wamara (48) aliyekuwa afisa kilimo na mifugo kata ya Bwile.

Aidha ameongeza kuwa tayari jeshi la polisi limewatia mbaroni watu wanne kwa ajili ya kusaidia upelelezi wa mauaji hayo, huku msako mkali ukiendelea ili kuwabaini wote walio husika katika tukio hilo.

Akizungumzia suala la kufanyika msako wa wizi usiku katika kijiji tofauti lililo zua tafsiri tofauti miongoni mwa wakazi wa mkoa Kagera, kamanda Mayunga amesema kuwa ni vigumu kuwalazimisha watu kufanya shughuli zao usiku ama mchana, ilimradi wafuate taratibu za kutoa taarifa kwa ngazi tofauti za uongozi katika sehemu husika.

Miili ya marehemu hao watatu imehifadhiwa katika Dispensary ya Nkwenda ikisubiri mazishi yanayotazamiwa kufanyika keshoo (april 13) huku idadi kamili ya ng’ombe waliokuwa wakitafutwa ikiwa bado haijafahamika.
Na Mwanaharakati.

No comments: