Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
nchini kuhakikisha kuwa kesi za rushwa dhidi ya watu mbali mbali inazozipeleka
mahakama zinakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa kwa maana ya washitakiwa
kukutwa na makosa.
Aidha, Rais Kikwete ameitaka Taasisi hiyo kuwa karibu na
umma akisema kuwa TAKUKURU na umma ni sawa na maji na samaki kwa sababu Taasisi
hiyo haiwezi kufanikiwa bila ushirikiano na umma.
Rais pia amesema kuwa Serikali yake inakusudia kutunga
sheria ya kuwalinda watoa habari kwa TAKUKURU ili kufanikisha zaidi kazi ya
Taasisi hiyo.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Alhamisi, Julai 17, 2014,
kwenye siku yake ya kwanza ya ziara rasmi ya siku sita mkoani Ruvuma ambako
ameanzia ziara yake katika Songea Mjini.
Katika siku yake ya kwanza leo, Rais Kikwete ambaye
anafuatana na Mama Salma Kikwete, amezindua ghala kubwa la kuhifadhia chakula
lililojengwa na Wakala wa Taifa wa Kuhifadhji Chakula (NFRA), amezindua nyumba
za bei nafuu ambazo zimejengwa katika eneo la Mkuzo na Shirika la Taifa la
Nyumba (NHC), amefungua rasmi Ofisi za TAKUKURU za Mkoa wa Ruvuma na pia
amehutubia mkutano mkubwa wa hadhara kwenye Uwanja wa Majimaji wa Songea.
Akizindua ofisi hiyo ya TAKUKURU, Rais Kikwete ameipongeza
Taasisi hiyo kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikiboreka kila mwaka lakini
akasisitiza kuwa wakati umefika kwa TAKUKURU kufiksha mahakamani kesi zile
ambazo zina nafasi kubwa ya kutuhumiwa kukutwa na hatia. "ni vyema
tuhakikishe kuwa kesi zinazokwenda mahakamani zinakuwa na mpangilio mzuri na
nafasi kubwa ya Serikali kushinda kesi hizo."
Ameongeza Rais Kikwete: "Ni vyema pia kuwa pamoja na
mafanikio yote ya TAKUKURU ni lazima taasisi hiyo iongeze ushirikiano wake na
umma. TAKUKURU na umma ni sawa na samaki na maji kwa sababu kama ilivyo kuwa
samaki hawezi kuishi nje ya maji, hivyo hivyo TAKUKURU haiwezi kufanikiwa bila
ushirikiano na umma, bila kupata habari kutoka umma."
Ofisi hiyo ya TAKUKURU ya Mkoa wa Songea imegharimu sh. bilioni
1.18 na imejengwa kwa kiasi cha miezi 20 ikiwa ni sehemu ya sera ya Serikali ya
kujenga ofisi tatu za mikoa kila mwaka ili kuondoa uhaba wa ofisi za kufanyika
kazi za Taasisi hiyo.
Kwenye uzinduzi za nyumba za NHC, Rais Kikwete ameambiwa
kuwa katika eneo hilo la Mkuzo, shirika hilo limejenga kiasi cha nyumba 18 za
kuuza na zimejengwa kwa gharama ya sh. milioni 676.
Rais Kikwete pia ameambiwa kuwa nyumba hizo zimejengwa
katika kutekeleza kaulimbiu ya NHC ya "Nyumba yangu, Maisha yangu"
ambayo mpaka sasa inatekelezwa katika mikoa 14. Ujenzi wa nyumba hizo
ulianza Januari mwaka jana na unakamilika mwezi ujao, Agosti, 2014.
Nyumba hizo, ameambiwa Rais Kikwete, kuwa zitauzwa kwa
gharama ya kati ya sh. milioni 33 na 44 bila kodi ya VAT lakini ambayo
inaongezeka na kuwa kati ya milioni 44 na 52 kwa kutegemea ukubwa wa nyumba -
kuanzia ya vyumba viwili hadi nyumba vitatu. Rais Kikwete anaendelea na
ziara yake mkoani humo.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment