Nicolaus Mac (None Association Movement) KWA MATANGAZO YA REDIO NA TV WASILIANA NASI KWA +255767814844- nicolausngaiza@gmail.com.
Monday, 18 August 2014
NEWS ALERT!!! TANZANIA HAKUNA EBOLA
Dkt. Chacha Mung’aho ambaye ni Afisa Afya Mkuu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii anayeshughulikia maeneo ya Bandari, Viwanja vya ndege na mipakani akizungumzia namna walivyojipanga kukabiliana na tishio la ugonjwa wa Ebola kupitia wasafiri wanaoingia nchini Tanzania amesema kuwa tayari Serikali imetenga maeneo maalum, vifaa vya uchunguzi na huduma kwa wasafiri watakaobainika kuwa na dalili za maambukizi ya ugonjwa huo.
Amesema kuwa wataalam waliopo kutoka Wizara ya Afya wanaendelea kushirikiana na wenzao wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege, Uhamiaji na Wizara ya Kilimo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuendesha zoezi la uchunguzi wa afya ili kupata taarifa za wasafiri kulingana na mataifa wanayotoka.
“Kwa sasa tunafanya kazi kwa kushirikiana na tunapata taarifa sahihi za abiria kutoka kwa mashirika ya ndege wanayotumia kusafiria jambo linalotusaidia kuwabaini wasafiri waliotoka katika nchi za Liberia, Ivory Coast na Guinea zilizoathiriwa na ugonjwa huo” Amebainisha Dkt. Chacha.
Amesema tangu kugunduliwa kwa ugonjwa huo mwezi Machi mwaka huu huko Afrika Magharibi mataifa mbalimbali duniani kote yamekuwa katika mapambano kudhibiti ugonjwa huo kuendelea kusambaa na kuleta maafa katika maeneo mengine duniani ambako haujafika.
Amesema serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari juu ya namna ya kujikinga na kuchukua tahadhari na endapo watabaini uwepo wa mtu mwenye dalili za Ebola pia kuratibu mipango yote ya vifaa tiba,matibabu na mazishi endapo ugonjwa huo utaingia nchini kupitia kamati ya maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu .
Aidha, amesema licha ya ugonjwa huo kuibuka na kupotea katika vipindi tofauti katika mataifa mengine ya bara la Afrika na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda , wataalam hapa nchini wanaendelea kufanya utafiti juu ya chanzo kinachohifadhi Virusi hao kutokana na tabia yao ya kupotea katika kipindi fulani na kuibuka tena.
Na Mwanaharakati.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment