Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amerejea
nchini jana kutoka visiwa vya Samoa ambako alimuwakilisha Rais Jakaya Mrisho
Kikwete kwenye Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kwa nchi za Visiwa.
Katika hotuba yake kwenye mkutano huo Dk. Shein
alisisitiza msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunga mkono
malengo ya mkutano huo ambayo ni kuleta maendeleo endelevu katika nchi za
visiwa kwa kuweka mkakati madhubuti kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabianchi katika nchi hizo.
Alieleza
pia haja ya ushirikiano thabiti na wa vitendo kutekeleza Malengo ya Milenia
ambayo bado hayafikiwa katika kipindi cha ajenda ya maendeleo baada ya mwaka
2015.
Aliwahakikishia wajumbe wa mkutano huo kuwa Rais
Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Afrika
kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi atasisitiza msimamo wa bara la Afrika katika
mkutano ujao wa kilele kuhusu mabadiliko ya Tabaianchi unaotarajiwa kufanyika
tarehe 23 Septemba 2014.
Akiwa visiwa vya Samoa, Dk. Shein alihudhuria pia uzinduzi
wa Mpango wa Magharibi ya Bahari ya Hindi wa Changamoto za Ukanda wa Pwani na
Mabadiliko ya Tabianchi ambapo aliuelezea mpango huo kuwa ni chombo muhimu
katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika ukanda huo.
Dk. Shein
alipata fursa ya kufanya mazungumzo kwa nyakati toafauti na Rais wa shelisheli
Mheshimiwa James Michel na Rais wa Comoro Mheshimiwa Ikililou Dhoinine.
Katika
mazungumzo hayo viongozi hao walizungumzia suala la kuimarisha uhusiano na
ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hizo.
Mbali ya viongozi Dk. Shein alikutana pia na Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Biashara (ITC) chenye makao yake mjini
Geneva Uswizi ambapo Mkurugnezi huyo alimueleza Rais kuwa kituo chake kiko
tayari kuisaidia Zanzibar kutekeleza mkakati wake wa kuongeza ajira kwa vijana
na kinamama kwa kutumia rasilimali zilizopo Zanzibar.
Katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Abeid Amani
Karume Dk. Shein alipokelewa na viongozi mbali mbali wa chama na serikali
wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi na Spika wa
Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho.
Miongoni
mwa wajumbe waliofuatana na Dk. Shein ni pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa Dk. Mahadhi Juma Maalim, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makanu wa Kwanza wa Rais Fatma Abulhabib Ferej na Mshauri wa Rais
Ushirikiano wa Kimataifa, Uchumi na Uwekezaji Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa
Wengine ni
Kaimu Naibu Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa Andy Mwandembwa, Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira katika Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais Sheha Mjaja Juma na mtaalamu wa mazingira kutoka Ofisi
ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Suleiman Kisimbo.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment