Serikali imekamilisha ukarabati na upanuzi wa uwanja
wa ndege wa Mpanda, mkoa wa Katavi na hivyo kuufanya uwe wa kiwango kizuri
tayari kwa kutumika kwa ndege za binafsi na biashara.
Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda, Bw Seneti Lyatuu
alisema uwanja huo umeboreshwa na hivyo, unaweza kutumika kutua na kuruka ndege
za kiwango cha kati na hata zile ndege kubwa zinaweza kutua kwa dharura.
Aliiambia timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoa
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango iliyotembelea uwanja huo mwishoni mwa wiki kuwa
uwanja huo umeongeza idadi ya wasafiri mara dufu kutokana na ukarabati na
upanuzi uliofanyika.
Meneja wa Uwanja huo alisema idadi ya abiria
imeongezeka kutoka abiria 285 mwaka 2009 hadi 2,390 mwaka 2013/14.
Timu ya ukaguzi ikitazama barabara ya kutua na kurukia ndege katika uwanja wa ndege wa Mpanda |
Bw. Lyatuu alisema kuwa uwanja huo umekarabatiwa na
barabara ya kuruka na kutua ndege imerefushwa kwa kiwango cha lami kutoka urefu
wa mita 1,500 na upana wa mita 30 hadi kufikia urefu wa mita 1,820 na upana wa
mita 30.
Alisema maeneo mengine yaliyokarabatiwa ni pamoja na
kujenga uzio na mifereji ya kupitishia maji ya mvua.
“Kwa sasa kiwanja kipo vizuri na ndege za aina zote
zinaweza kutua hapa uwanjani hivyo, tunawakaribishwa wadau wote kuutumia uwanja
huu” alisema Bw Lyatuu.
Eng. Caroline Mntambo kutoka Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Makao Makuu Dar es Salaam alisema kuwa tayari wamealika mashirika ya
ndege yanayofanya biashara hapa nchini kuanzisha safari katika uwanja huo.
Mashirika hayo ni pamoja na ATC, Precision Air, Fast jet nk.
Eng Mntambo alisema kwa sasa shirika la ndege la Auric
Air tayari limeanzisha safari za kwenda Mpanda ambapo linasafirisha abiria
kutoka Dar- Mpanda – Mwanza mara tatu kwa wiki.
Alisema ndege zingine zinazotua uwanjani hapo kwa sasa
ni pamoja na za UNHCR, ndege za kukodi na ndege za serikali.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment