Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa maendeleo ya haraka ya Jamhuri ya Watu wa
China ni hamasa kubwa na ya kutosha kwa nchi za Afrika kuwa nazo zinaweza
kuendelea katika kipindi kifupi kama zitaongozwa na sera sahihi za mageuzi ya
kiuchumi.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Ijumaa, Oktoba 24,
2014, wakati alipokutana kwa mazungumzo rasmi na Mwenyekiti (Spika) wa Bunge la
Jamhuri ya Watu wa China, National People’s Congress (NPC) Mheshimiwa Zhang
Dejiang, ikiwa ni moja ya shughuli za Mheshimiwa Rais katika ziara yake rasmi
ya China.
Katika mazungumzo hayo kwenye Jengo la Bunge la Great
Hall of the People mjini Beijing, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Dejiang: “China inatuhamasisha sana kwamba na sisi
tunaweza kupata mabadiliko na maendeleo ya haraka ya wananchi wetu ili mradi tu
tuweze kuwa na sera sahihi ambazo zinalenga katika kuleta mageuzi ya msingi na ya
kweli kweli ya kiuchumi”.
Rais Kikwete amesema kuwa kwake yeye ambaye amekuwa
anatembelea China kila baada ya wastani wa miaka minne, mabadiliko ya China
yanatia hamasa kweli kweli kuwa nchi za Afrika pia zinaweza kuleta mageuzi
makubwa ya maisha ya watu wake.
“Nilikuja
hapa kwa mara ya kwanza mwaka 1980, na tokea wakati huo nimetembelea nchi hii
kila baada ya miaka minne kwa wastani na kila nikija nashuhudia mabadiliko
makubwa yasiyopimika na wala kufikirika.
China ilikuwa nchi masikini sana
wakati nilipofika hapa kwa mara ya kwanza lakini katika miaka 30 tu imebadilika
kutoka nchi masikini na kuwa nchi iliyoendelea na yenye uchumi unaoshikilia
nafasi ya pili kwa ukubwa duniani,” amesema Rais Kikwete
na kuongeza:
“Tunawapongeza
sana kwa juhudi ambazo zimewafikisheni hapa. Mnatuhamasisha na sisi kuwa ipo
siku moja na sisi katika Afrika tutafikia hatua hii ya maendeleo.”
Naye Mheshimiwa Dejiang amemkubusha Rais Kikwete
mazungumzo kati yao wakati walipokutana kwa mara ya kwanza miaka saba iliyopita
Ikulu, mjini Dar es Salaam.
Wakati huo, Mheshimiwa Dejiang alikuwa Katibu wa
Chama Tawala cha Kikomunisti cha China katika Jimbo la Guangzhou, jimbo ambalo
linaongoza katika China kwa kufanya biashara na Tanzania. Kati ya biashara zote
ambazo Tanzania na China zinafanya, asilimia 60 inatokea Jimbo la Guangzhou.
Mheshimiwa Dejiang pia amepongeza mahusiano mazuri
kati ya Tanzania na China katika miaka 50 tokea nchi hizo mbili kuanzisha
uhusiano wa kibalozi Aprili 26, mwaka 1964.
Mwenyekiti huyo wa Bunge pia amesema kuwa ujenzi wa
Reli ya TAZARA unaendelea kuthibitisha urafiki baina ya watu wa China, Tanzania
na Zambia na kuongeza kwa Tanzania kwa kuimarisha TAZARA na kwa kutilia maanani
utajiri na raslimali zilizopo, ikiwemo nafasi ya kijiografia, utulivu na amani
na idadi kubwa ya watu, Tanzania ina sifa ya kuwa nchi tajiri katika miaka
isiyokuwa mingi ijayo.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment