Mkutano wa
kitaalamu ambao unawakutanisha wataalamu mbalimbali kutoka tasnia za mipango,
uchumi, takwimu na maendeleo, wenye wajibu wa kusimamia uchumi na mipango
umefunguliwa rasmi na kuwakutanisha kwa pamoja wakurugenzi wa sera na mipango,
maafisa mipango kutoka kwenye wizara, Serikali za Mitaa, idara na wakala wa
Serikali, pamoja na taasisi za kitaaluma na watafiti wanaojishughulisha na
masuala ya maendeleo na uchumi.
![]() |
Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango akisoma hotuba wakati wa mkutano wa mwaka wa wachumi na maafisa mipango unaofanyika jijini Dar es Salaam. |
![]() |
Washiriki wa mkutano wa mwaka wa wachumi na maafisa mipango wakimsikiliza Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Hayupo pichani). |
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Balozi (Mstaafu) Dkt. Lumbanga
alisema kuwa wachumi na maafisa
mipango wana wajibu mkubwa katika kuishauri serikali juu ya njia bora na
madhubuti za kupambana na umaskini na kuharakisha maendeleo kwa jamii ya
Watanzania.
“Muna dhima
kubwa katika kushauri kitaalamu juu ya namna nzuri za kupunguza tatizo sugu la
umaskini miongoni mwa Watanzania,” alisema.
Balozi
(Mstaafu) Dkt. Lumbanga aliwasihi
washiriki kutumia fursa hiyo kujadili kwa kina na kubadilishana uzoefu juu ya
sera, mipango na kujenga mtandao wa masuala ya maendeleo ya kitaaluma.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kutoa fursa ya kuwakutanisha kwa pamoja
wataalamu hao na kujenga uelewa wa pamoja juu ya uendeshaji wa shughuli
mbalimbali za Serikali.
Aliongeza
kuwa Mkutano huo, unatoa fursa za kujadiliana kwa pamoja juu ya mafanikio na
njia za kukabiliana na changamoto kwa kubadilishana uzoefu na ujuzi kwenye
masuala hayo.
“Mkutano
huu ni muhimu katika kuimarisha utendaji kazi wa kada hizi kwa minajili ya
kusukuma gurudumu la maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini,” alisema Dkt.
Mpango.
Kwa mujibu
wa ratiba ya mkutano huo, Mada mbalimbali zinawasilishwa kwa kutilia mkazo
masuala mbalimbali ya kimaendeleo yanayojitokeza hivi sasa, ambapo mkutano huo
unajadili masuala ya Maendeleo ya Tasnia ya Wapanga Mipango (wachumi, maafisa
mipango na watakwimu) na Maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (2015/16 – 2020/2021).
Mada
nyingine ni pamoja na Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji katika Sekta ya Umma
ambao una lengo likiwa kuimarisha utendaji, ufanisi na uwajibikaji katika
matumizi ya rasilimali za umma zilizotengwa kwa ajili ya miradi na program za
maendeleo. Pamoja na mada ya Namna bora ya kujiandaa na Uchumi wa Gesi.
Washiriki
wa mkutano huu ni pamoja na wakurugenzi wa sera na mipango, maafisa mipango
kutoka kwenye wizara, Serikali za Mitaa, idara na wakala wa Serikali, pamoja na
taasisi za kitaaluma na watafiti wanaojishughulisha na masuala ya maendeleo na
uchumi.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment