Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesisitiza kuwa ni wajibu wa wakuu wa mikoa na wilaya kupanga ratiba maalum za
kutembelea wananchi mara kwa mara kusikiliza matatizo yao na kuyatafutia
ufumbuzi.
Amesema
kazi ya Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya si ya kukaa ofisini tu bali ni kazi ya
kushughulikia matatizo ya wananchi kwa kuwatembelea kusikiliza shida zao,
kusikiliza maoni yao na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto
mbalimbali zinazowakabili.
Akihitimisha
mkutano wa siku moja na wakuu wa Mikoa na Wilaya za Unguja na Pemba uliofanyia
Ikulu jana, Dk. Shein aliwataka watendaji wakuu hao wa Mikoa na Wilaya
kufanyakazi kwa kujiamini na kamwe wasiwakimbie wananchi.
“msikae
maofisini, pangeni ratiba maalum… msiwakimbie wananchi, nendeni kwao
mkawasikilize na mkabiliane na matatizo waliyonayo”alisisitiza Dk. Shein na
kuongeza kuwa wanapokwenda huko hawana budi kujiandaa isiwe ni jambo la
kubahatisha.
Aliwaambia
kuwa ni wajibu wao kutoa majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi na pale
ambapo wanakosa majibu ya haraka waahidi kuyatolea majibu wakati mwingine.
Kuhusu
migogoro ya ardhi ambayo inaonekana kushamiri hivi sasa, Mhe Rais aliwaeleza
watendaji wakuu hao wa Mikoa na Wilaya kuwa wanapaswa kuwa majasiri katika
kubaliana nayo na wakati mwingine watalazimika kuchukua maamuzi magumu.
“Jukumu
letu ni kushughulikia mogogoro ya ardhi na muhimu zaidi tunapaswa kuzifahamu
sheria za ardhi na kuzitekeleza na endapo hatuzifahamu tunapaswa kuwaita
wataalamu wa sheria kutoka wizara husika kusaidiana kuitatua” Dk. Shein
alisisitiza.
Mhe
Rais aliwakumbusha wakuu hao wa Mikoa na wilaya kuwahakikisha watumishi wa
ofisi zao wanaelewa vyema majukumu ya Ofisi za Mikoa na Wilaya na hivyo hivyo
kwa wananchi wa mikoa na wilaya zao.
Aidha,
aliwataka kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini kwa kuwa uteuzi wao umefanyika
kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia sifa na weledi hivyo Serikali imeridhishwa
na uwezo wao wa kuzitumikia nyadhifa hizo.
“Serikali
inaamini kuwa kwa sifa zenu za utendaji kazi kitimu, kujituma kwenu,
kujiheshimu kwenu, uadilifu wenu na sifa nyenginezo mtakidhi matarajio ya
serikali na wananchi” Dk. Shein aliwaeleza.
Aliwaambia
kuwa kazi yao kubwa ni kubadilii mazingira ya mikoa na wilaya wanazoziongoza na
wataweza kufanya hivyo kama wataimarisha mashirikiano na watumishi walio chini
yao na wananchi kwa jumla.
Kwa
hivyo alihimiza kuweka utaratibu wa vikao vya kawaida vya kila ngazi katika
ofisi zao ili masuala mbalimbali yanayohusu ofisi na watumishi yaweze
kuzungumzwa na kama ni changamoto ziweze kutafutiwa ufumbuzi kwa pamoja.
Katika
mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na
Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Joseph Meza,
Dk Shein alisisitiza pia umuhimu wa wakuu wa Mikoa na Wilaya kutafuta ushauri
au kukubali kushauriwa kwa kuwa hiyo ni njia mojawapo ya kuimarisha uongozi wa
pamoja katika sehemu zao za kazi.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu Kiongozi na Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliwakumbusha
wakuu wa Mikoa na Wilaya kutumia utaratibu uliowekwa na Serikali wa kuwasiliana
na wananchi.
“ni
lazima tuutumie utaratibu uliowekwa na serikali wa kuwasiliana na wananchi mara
kwa mara ili kuwaeleza masuala mbalimbali ya serikali ikiwemo utekelezaji wa
programu mbalimbali za maendeleo” alisema Dk. Abdulhamid.
Alibainisha
kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza kwa mafanikio makubwa miradi mbalimbali ya
maendeleo lakini wananchi hawakosa taarifa muhimu za miradi hiyo kutokana na
viongozi kutowasiliana nao mara kwa mara.
Katika
mnasaba huo, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Baraza la
Mapinduzi aliwataka wakuu hao kutembelea maeneo yao ya kazi kijiji kwa kijiji
ili kuyafahamu na pia kupata fursa kukutana na wananchi.
“Ni
muhimu uwepo wa Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya uonekane katika kila eneo la
mkoa na wilaya ili wananchi wamfahamu na waweze kuwasiliana nae” Dk. Abdulhamid
alisema.
Aliwaeleza
kuwa ni muhimu kwao kujiwekea lengo la kufanya jambo kubwa angalau moja la
maendeleo litakalokuwa kumbukumbu nzuri ya uongozi wao na kuwafanya wananchi
wawakumbuke watakapomaliza utumishi wao katika mikoa na wilaya walizoziongoza.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment