Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za
Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Rajabu Rutengwe kuomboleza vifo
vya watu 11 ambapo wengine kadhaa walijeruhiwa katika ajali ya barabarani
iliyotokea tarehe 27 Novemba, 2014.
Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mkanyageni Mkoani Tanga baada ya basi dogo aina ya Toyota Coaster Na. T 410 BJD iliyokuwa ikitoka Tanga Mjini kuelekea Lushoto kugongana na Lori aina ya Scania Na. T 605 ABJO.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya
kupotea ghafla kwa maisha ya watu 11 na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali ya
barabarani iliyotokea katika Mkoa wako wa Tanga”, amesema Rais Kikwete katika
Salamu zake na kuongeza:
“Naomba upokee salamu zangu za rambirambi
kutoka dhati ya moyo wangu kutokana na vifo hivyo, na kupitia kwako, naomba
salamu za pole ziwafikie watu wote waliopotelewa na ndugu na jamaa zao kwenye
ajali hiyo”.
Rais Kikwete amesema
anawaomba wote waliopoteza ndugu na jamaa zao kwenye ajali hiyo wawe watulivu
na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, na amewahakikishia
kuwa yuko pamoja nao katika kipindi chote cha maombolezo.
“Kwa wote waliojeruhiwa
kwenye ajali hiyo, namwomba Mungu awajalie ahueni na wapone haraka, ili warejee
tena katika hali zao za kawaida. Namwomba Mola azipokee na kuzilaza mahala pema
peponi Roho za Marehemu wote, Amina”, amemalizia kusema Rais Kikwete katika
Salamu zake.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment