MAC PRODUCTION STUDIO'S

MAC PRODUCTION STUDIO'S
KWA MATANGAZO YA BIASHARA REDIONI( 0767-814844)

Wednesday, 3 December 2014

NEWS ALERT!!! TGNP: NGUVU YA PAMOJA ITASAIDIA KUPUNGUZA UKATILI WA KIJINSIA



Lengo kuu la siku hizi 16 ni  kuendeleza mijadala, kutafakari kwa pamoja  kuhusu mikakati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia, mafanikio yake, changamoto na namna ya  kujipanga na kusonga mbele kwa pamoja.  Kila mwaka kunakuwa na kauli mbiu na kauli mbiu ya mwaka huu hapa Tanzania ni “Funguka! Fichua Ukatili kwa afya ya jamii” Hii ina maana kuwa tuvunje ukimya kila tunaposhuhudia kitendo chochote cha ukatili wa kijinsia tuchukue hatua.  Aidha kauli mbiu itayoongoza mjadala wetu wa leo ni  “Siyumbishi, Najilinda Mnilinde” kauli mbiu hii inalenga vijana kwani tunaamini kuwa mapambano haya yanahitaji nguvu kubwa na ya pamoja. Vijana  ni zaidi ya 60% ya watanzania wote. Hii ni idadi kubwa sana.

Tunatarajia   hawa vijana ndio watakaoendesha taifa hili kwa miaka hamsini ijayo  hivyo basi mikakati yetu lazima iwalenge vijana. Vijana  hususan vijana wa kike wanakabiliwa pia  na ukatili wa kijinsia kwa kiasi kikubwa. Hivyo  basi   wanatakiwa kujilinda  dhidi ya mazingira hararishi ambayo yanaweza kuwasababishia kukumbana na ukatili wa kijinsia.  Jamii pia inajukumu kubwa la  la kuwalinda vijana  katika kuwatayarishia mazingira bora  dhidi ya ukatili wa kijinsia kuanzia nyumbani, shuleni vyuni hadi maofisini.

 Tatizo la jira ni kubwa  sana  na kwa kiasi kikubwa linasababisha ukatili kwa wasichana  hususan ule wa ajira zisizo na utu,  usafirishaji  haramu wa wasichana, biashara ya ngono,  rushwa ya ngono , ndoa za utotoni n.k. Tunasisitiza uwepo wa  mabweni ya kutosha katika shule zote za sekondari za kata na nyigine hususan ya wasichana ili kupunguza umbali  na mazingira hatarishi kwenda shuleni.

"Tunatarajia kuwa baada ya mjadala huu vuijana wetu watakuwa mabalozi wa kupinga ukatili wa kijinsia na kuitekeleza kauli mbiu hii  ya kutokuyumbisha, kujilinda na jamii kuwalinda".

Ndugu mgeni rasmi, TGNP kwa kushirikina na wadau wengine  tunaungana na wenzetu  kote duniani kupinga ukatili wa kijinsia. Mapambano haya yameanza muda mrefu japokuwa hali bado si nzuri kwani  takwimu  zinaonesha kwamba 1/3 ya  wanawake waliona umri kati ya miaka 15 – 49  wamefanyiwa ukatili wa kijinsia na wenzi au ndugu zao. Wanawake 2 kati ya 5  wamefanyiwa ukatili tangu wakiwa na miaka 15. Asilimia 44  ya wanawake walio katika ndoa kati ya umri wa miaka 15-49  wamefanyiwa ukatili na wenzi wao.  20% ya wanawake  wenye umri kati ya miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kingono na wapenzi wao.

 Takwimu za  wizara ya afya zinaonesha, katika mwaka 2013 asilimia 23% ya wasichana wenye umri kati ya miaka 15 na 19 walikuwa na mimba au walikuwa na watoto huku zikionesha kuwa asilimia 18% ya wasichana wa umri huo huolewa utotoni.  Wasichana 4  kati ya 10 ni wahanga wa mimba za utotoni.  Mwaka 2012 wasichana 8000 waliacha shule kutokana na mimba za utotoni na kati ya hao 3000 walikuwa shule za msingi. Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa bado ukeketaji ni tatizo kubwa likiwa bado linatendeka kwa asilimia 15%.  Pia  asilimia 14.6 ya wanawake  wa Tanzania wamefanyiwa  ukeketaji. Mikoa inayoongoza kwa ukeketaji ni  manyara 70.8%, Arusha 58.6% na  Mara 39.0% ( 2010).Hali hii inatisha na inahitaji  nguvu ya ziada  ili kukomesha ukatili huu.
 

Na Mwanaharakati.

No comments: