
HATIMAYE Mkurugenzi
wa Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam, Alex Msama, ameibuka na
kutamka yeye si Meneja wa malkia wa nyimbo za injili nchini, Rose Muhando
akisema amekuwa akishirikiana naye katika mazingira ya kawaida kama ilivyo kwa
waimbaji wengine.
Kwa mujibu wa taarifa
ya Msama kwa vyombo vya habari jana, yeye akiwa mlezi wa waimbaji wote wa
muziki wa Injili, amekuwa akishirikana nao kwa karibu kutokanana nafasi yake
katika huduma hiyo ya uimbaji kwa kipindi cha miaka 15.
Msama, mtu
aliyechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya muziki wa injili nchini kutokana na
kuandaa matukio ya muziki huo kama Tamasha la Pasaka, uzinduzi wa albamu na
Tamasha la Krismas, alisema ameamua kutoa tamko hilo kutokana na malalamiko ya
muda mrefu ambayo amekuwa akipata juu ya Rose.
"Nimekuwa
nikipokea malalamiko mengi ikiwemo kutoka kwa viongozi wa kiroho wakiwemo
wachungaji, kwamba pengine nimekuwa nikimzua Rose (Muhando) katika mtamasha
wanayomualika na kushindwa kutokea.
"Lakini, naomba
watumishi wa Mungu wanielewe katika hili, sipokei mialiko wala simzuii Rose.
Mimi ninapokuwa na matamasha, nimekuwa nikimualika kama wafanyavyo wengine.
"Nimekuwa
nikimlipa kiasi cha fedha anachotaka na hakuna zaidi, hivyo mimi sio Meneja
wake," alisema Msama katika taarifa hiyo na kuongeza:
"Agosti mwaka
huu, kampuni yangu ilidhamini uzinduzi wa albamu yake ya Kamata Pindo la Yesu,
haikuwa na maana kwamba ni Meneja wake.
"Nilimualika
uzinduzi wa albamu ya Uko Hapa ya msanii John Lissu Oktoba mwaka huu, nilimlipa
fedha, lakini hakutokea kama ambavyo amekuwa akifanya kwa wengine ambao
wamekuwa wakilalamikia tabia hiyo," alisema Msama.
"Pia wiki
iliyopita nilikuwa na Tamasha la Krismasi tulikubaliana aje katika maonesho
hayo, lakini hakutokea na tulishamlipa," alisema Msama kwa masikitiko na
kuongeza kuwa amemsamehe na anamuombea kwa Mungu aweze kubadilika.
Alieleza kuwa hana
tatizo na mwimbaji huyo, wala hana ugomvi naye, lakini amekuwa akipata taabu
kutoka kwa baadhi ya wachungaji pale Rose anapoalikwa halafu hatokei na inaonekana
yeye ndiye amemzuia.
"Sijawahi
kupokea mialiko kwa niaba ya Rose, kila kitu anafanya mwenyewe, hivyo ni vyema
wadau wakafahamu hilo," alisema Msama na kusema angekuwa mwepesi wa
kulalamika, angeshafanya hivyo muda mrefu dhidi ya Rose.
Aidha, Msama amekana
kuhusiana na madai ya Rose kutumia dawa za kulevya na kusisitiza kuwa hajawahi
kumuona akijidunga kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti
na kuongeza kama ikiwa ni kweli, hilo pia ni suala binafsi.
"Baadhi ya
vyombo vya habari vinaandika ni mjamzito, nafikiri pia hayo ni mambo yake
binafsi na hakuna mtu mwenye haki au uhalali wa kuhoji hilo.Yule ni mtu mzima
na mwenye kujielewa," alisema Msama.
Rose ni mwimbaji
mahiri wa muziki wa injili nchini aliyejipatia sifa ndani na nje ya ukanda wa
Afrika Mashariki ambaye mwishoni mwa mwaka 2013, alisaini mkatabawa kufanya
kazi na kampuni ya muziki ya Sony ya Afrika Kusini.
Miongoni mwa albamu
zilizompa umaarufu Rose kiasi cha kuwa alama ya mafanikio ya muziki wa injili
nchini, ni 'Uwe Macho,' Nyota ya Ajabu (Zawadi ya Krismasi), Jipange Sawasawa,
Kitimutimu, 'Mungu Anacheka' na Wololo na Kamata Pindo la Yesu aliyoachia hivyo
karibuni.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment