Kufuatia kukamilika kwa mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Serikali za
Mitaa, Vijiji na Vitongoji na hivi sasa kuendelea kwa zoezi la kuapishwa kwa
viongozi hao katika maeneo mbalimbali hapa nchini, kumejitokeza tabia ya baadhi
ya wananchi kufanya vurugu na fujo katika zoezi hilo.
Baadhi ya wananchi wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kihalifu kwa
kufanya fujo na vitendo vya vurugu ikiwemo kuwapiga baadhi ya watendaji
wanaosimamia zoezi la kuapisha na kuwapiga viongozi wateule waliochaguliwa
kihalali na wananchi kwa madai kuwa hawakushinda kihalali katika uchaguzi huo
jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini, linatoa onyo kwa wananchi wenye
tabia hiyo kuacha mara moja na badala yake kama mtu hakuridhika na matokeo ya
uchaguzi huo, afuate utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yake kwenye ngazi
husika ili yaweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Jeshi la Polisi linawata Wakurugenzi na Maafisa watendaji wenye
dhamana ya kusimamia mchakato wa kuwaapisha wenyeviti waliochaguliwa, kufuatilia
kwa karibu migogoro inayojitokeza na kuitatua migogoro hiyo mapema ili kuepusha
migongano inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Jeshi la Polisi halitamvumilia mtu ama kikundi chochote kitakachofanya vurugu
ama fujo kwa kisingizio cha ushabiki wa siasa na badala yake atakayebainika
hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Imetolewa na:
Advera J. Bulimba - SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment