Watu10 wa jijini Tanga, akiwemo
mwanafunzi wa sekondari wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
wakikabiliwa na makosa matano tofauti kuhusu tukio la kuwanyang’anya polisi
silaha pamoja na kumuua askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ),
Sajenti Mohamed Rashid Kajembe.
Mwanafunzi aliyefikishwa mahakamani
ni Rajab Bakari (19) wa shule ya sekondari na mkazi wa Makorora jijini humo.
Watuhumiwa tisa wameelezwa kuwa ni
wafanyabiashara............
, nao ni Mbega Seif (25) maarufu ‘Abuu Rajab’ mkazi wa Kiomoni,
Amboni, Ayubu Ramadhani (27) maarufu ‘Chiti’ ambaye ni fundi umeme na mkazi wa
Kona Z Kiomoni, Hassani Mbogo (20) maarufu ‘Mpalestina’ mkazi wa Makorora,
Mohamed Ramadhani (19) mfanyabiashara na mkazi wa Makorora, Sadiki Mdoe (25)
maarufu ‘Kizota au Kisaka’ mkazi Magaoni.
Washtakiwa wengine ni Saidi Omari
(26) mkazi wa Magaoni Tairi Tatu, Nurdin Mbogo (27) Makorora, Ramadhan Mohamed
(18) mkazi wa Donge pamoja na Omari Harubu Abdala (55) maarufu ‘Ami’ mkazi wa
Dunia Hoteli Makorora.
Wakisomewa mashtaka yao mbele ya
Hakimu Mkazi Aziza Rutala, Wakili wa Serikali, George Barasa akisaidiana na
MariaClara Mtengule, walidai kuwa kosa la kwanza hadi la tatu linawahusisha
washitakiwa namba moja mpaka nane (1 -8) ambao wanatuhumiwa kushiriki kula
njama ya kutenda kosa kinyume cha sheria.
Barasa alidai kuwa katika maeneo
tofauti ya jijini Tanga kati ya Septemba mosi 2014 hadi Januari 26 mwaka huu,
washitakiwa wote wanane kwa pamoja walitenda kosa la kula njama na kufanya kosa
la unyang’anyi wa silaha.
Katika kosa la pili, Barasa alidai
mahakamani hapo kwamba mnamo Januari 26 mwaka huu, katika mgahawa wa Jamali
ulipo kati ya barabara ya Nne na ya Tano jijini Tanga, washitakiwa wote wanane
waliiba silaha moja aina ya SMG namba za usajili 14303545 mali ya Polisi na
muda mfupi kabla ya kutenda kosa hilo walitumia visu kumchoma askari H 501
Mwalimu ili kupata silaha hiyo.
Kosa la tatu la washitakiwa hao ni
unyang’anyi wa kutumia silaha, na washitakiwa wote wanane wanadaiwa kuwa katika
mgahawa wa Jamali uliopo kati ya barabara ya nne na ya tano waliiba silaha
nyingine yenye namba za usajili 14301230 SMG mali ya polisi na kwamba muda
mfupi kabla ya kutenda kosa hilo walimtishia kwa kutumia nguvu kumnyang’anya
silaha PC H Mansoor kinyume na sheria.
Hata hivyo, katika kosa la nne
ambalo limemhusisha mshitakiwa namba tisa Nurdin Mbogo wakili huyo wa Serikali,
alidai kuwa Februari 6 mwaka huu, katika sehemu isiyofahamika jijini Tanga,
mshtakiwa huyo akijua kuwa Hassan Mbogo (Mshitakiwa Na. 4) alitenda kosa
Septemba mosi 2014 na Januari 26 mwaka huu alimsaidia kumwezesha kukwepa
kushtakiwa na kuadhibiwa kinyume na sheria.
Katika hatua nyingine, Wakili wa
Serikali Mtengule alisoma shitaka jingine jipya ambalo liliwahusisha watuhumiwa
watatu akiwemo namba 1 na 2 (Mbega Rajabu na Rajabu Bakari) pamoja na mshtakiwa
mwingine Omari Harub Abdallah ‘Ami’ wakidaiwa kwa pamoja kuhusika kumuua askari
wa JWTZ, Sajenti Mohamed Rashid Kajembe mnamo Februari 13 mwaka huu katika
Mapango ya Amboni Jijini Tanga kinyume cha sheria namba 196 na 197 ya makosa ya
adhabu ya mwaka 2002 .
Washtakiwa hao watatu hawakutakiwa
kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi
hiyo ya mauaji.
Hata hivyo, washitakiwa wote 10 kwa
pamoja wamekana makosa yao, na mahakama imewanyima dhamana washitakiwa tisa
kutokana na makosa waliyotenda kutokuwa na dhamana.
Mshitakiwa namba tisa Nurdin Mbogo
alishindwa kutimiza masharti ya dhamana baada ya kutakiwa kutoa Sh milioni moja
na mdhamini mmoja mwenye mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni moja.
Washitakiwa wote wamerudishwa
rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Machi 23 mwaka huu kwa kuwa upelelezi
wake haujakamilika.
Mnamo Februari 13 mwaka huu katika
eneo la Amboni Jijini Tanga palizuka mapigano baina ya askari polisi
wakishirikiana na JWTZ dhidi ya watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi, waliokuwa
wamejificha kwenye mapango ya Majimoto.
Katika tafrani hiyo, kulisababish
kifo cha askari wa JWTZ na majeruhi watano wakiwemo wanajeshi wawili na Polisi
watatu, hali iliyozua hamaki kwa wakazi wa jijini hapa.
Rais Jakaya Kikwete katika hotuba
yake mwezi uliopita alielezea matukio hayo kuwa ni ya ujambazi, lakini pia yana
mwelekeo wa ugaidi na akalitaka jeshi la polisi kuwasaka watuhumiwa wote na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment