Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kuwasaka na
kuwarudisha shule kiasi cha wanafunzi 6,000 ambao wamefaulu kwenda sekondari
mwaka huu, lakini hawako shule, na hawajulikani walipo.
Rais Kikwete alitoa maagizo hayo, jana, Machi 12,
2015 mjini Kahama alipopatiwa ripoti ya
maendeleo ya Mkoa wa Shinyanga wakati wa ziara yake maalum ya siku mbili kuwapa
pole wahanga wa mvua kubwa iliyonyesha usiku wa Machi 3, mwaka huu, na
kusababisha vifo vya watu 47 na uharibifu mkubwa wa nyumba, mali na mazao
katika vijiji vitatu vya Kata ya Mwakata, Wilaya ya Kahama, Mkoani Shinyanga.............
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Ali Lufunga,
alimwambia Rais Kikwete kuwa mwaka jana watoto 13,349 mkoani humo walishinda
mtihani wa kuingia kidato cha kwanza lakini hadi Februari 29, mwaka huu, ni
asilimia 56 ya watoto waliokuwa wamejiunga sekondari wakati asilimia 44, sawa
na watoto 5,913, hawajaripoti shuleni na hawajulikani walipo pamoja na ukweli
kuwa kitaifa kwa miaka mitatu mfululizo Mkoa huo umefanya vizuri kitaaluma.
Rais Kikwete ameuagiza Mkoa huo kutumia sheria
kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu wote, wakiwemo wazazi na walezi,
ambao wanahusika na utoro wa watoto hao.
“Hawa ni
watoto wengi sana na siyo jambo gumu kujua waliko. Hatuhitaji kujua sayansi ya
kutengeneza roketi ama undani wa sayansi ya nyuklia kuwasaka na kuwapata watoto
hawa. Shule walizosoma zinajulikana, walimu wakuu wa shule hizo wanajulikana,
wenyeviti wa vijiji wanakoishi wanajulikana, wazazi wao wanajulikana …hawa wote
watatoa habari walipo watoto hawa, tena katika muda mfupi tu wa wiki moja.”
Rais Kikwete ameongeza kuutaka uongozi wa Mkoa
kutokutoa visingizio vya kuhalalisha kushindwa kupatikana kwa watoto hao: “Katika
muda wa wiki moja, pateni taarifa za kila mtoto. Kama kuna wazazi wameoza
watoto wa kike wabanwe na kurudisha ng’ombe wa mahari, kama kuna waliooa watoto
hawa wa shule wakamatwe na kushitakiwa, kama watoto hawa wamekwenda kwenye
machimbo wasakwe huko huko…watafuteni watarudi tu.”
Katika Mkoa wa Shinyanga, kama ilivyo katika mikoa
karibu yote nchini, watoto wote ambao wanashinda mtihani wa kumaliza darasa la
saba, wanapata nafasi ya kuingia sekondari kwa sababu ya upanuzi mkubwa wa
elimu ya sekondari nchini na kuwepo kwa nafasi za kutosha kwa watoto wote
wanaoshinda mtihani.
Imetolewa
na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
– Dar es Salaam.
13
Machi, 2015
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment