.Yabaini silaha binafsi kutumika,
.Wahamiaji haramu kuingiza mifugo,
.Sasa kufungua mashauri na kufidia
patakapostaili.
Tarehe
01/05/2014, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
aliunda Tume ya Uchunguzi kuhusu malalamiko yaliyotokana na utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza. Aliteua Makamishna watatu ambao ni Mhe. Balozi Jaji (Mst)
Hamisi Amiri Msumi kama mwenyekiti wa tume, Mhe. Jaji (Mst) Stephen
Ernest Ntashima Ihema (Kamishna), Mhe. Jaji (Mst) Vincent Kitubio Damian
Lyimo (Kamishna) na Ndugu Frederick Kapela Manyanda kama katibu wa Tume.
Katika
uchunguzi huo, waziri Kagasheki aliyejiuzulu pamoja na wengine watatu
walioondolewa, hakuna aliyekutikana na hatia au kuhusika na utekelezaji wa
operation hiyo, ambayoiliundwa kuchunguza maeneo yaliyokumbwa.
Tume
imekamilisha kazi yake na kukabidhi taarifa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 10 Aprili, 2015. Kwa maagizo
ya Rais tumeisoma na kuichambua taarifa hiyo vya kutosha. Kwa hakika Tume
imefanya kazi kubwa sana, na nzuri sana ya uchunguzi na uandishi wa taarifa.
Kazi imefanywa kwa weledi na umakini wa hali ya juu na kwa lengo dhahiri la
kutenda haki. Katika siku 265, Tume ilitembelea wilaya 38 katika mikoa 20 na
kuhoji jumla ya mashahidi 259. Mikoa iliyohusika ni Kigoma, Katavi, Rukwa,
Mbeya, Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa,
Morogoro, Pwani, Tabora, Singida, Manyara, Arusha na Tanga.
Tume
imejitahidi kuwahoji wote waliokuwa na malalamiko, kuwahoji mashuhuda, kuwahoji
watuhumiwa, na kukusanya ushahidi wa aina mbalimbali ili ama kuthibitisha
makosa pale yalipofanyika na kupendekeza hatua za kuchukua, au kujiridhisha
kuwa tuhuma na malalamiko hayakuwa ya msingi. Kazi hiyo imefanywa vizuri na
kurahisisha kazi ya Serikali ya kuchukua hatua zinazostahili.
Operesheni Tokomeza ilivyotekelezwa
Tume
ilibaini kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja cha utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza iliyoanza tarehe 4 Oktoba, 2013, mafanikio mengi yalipatikana,
ikiwemo:
Watuhumiwa
1,030 wa makosa mbalimbali yanayohusu ujangili na uvunaji haramu wa misitu
walikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria;
Kukamatwa
kwa meno ya 211 yenye uzito wa kilo 522, meno ya ngiri 11, mikia ya wanyama
mbalimbali 36, ngozi za wanyama mbalimbali 21, pembe za swala 46, mitego ya
wanyama 134, ng’ombe 7,621 waliokuwa wanachungwa ndani ya hifadhi na misitu,
baiskeli 58, pikipiki 8 na magari 9;
Katika
kipindi cha Operesheni kulikamatwa jumla ya bunduki za kijeshi 18, bunduki za
kiraia 1,579, risasi 1,964, mbao vipande 27,913, mkaa magunia 1,242, magogo 858
na misumeno 60.
Operesheni
ilifanikiwa kupunguza kasi ya mauaji ya tembo kutoka tembo wawili kwa siku hadi
tembo wawili kwa mwezi wakati wa Operesheni;
Operesheni
ilisitishwa rasmi tarehe 01/11/2013 ili kupisha uchunguzi wa malalamiko
yaliyojitokeza. Baada tu ya kusitishwa kwa Operesheni wafugaji wengi
wamerudisha mifugo yao katika maeneo ya hifadhi yaani Mapori ya Akiba, Hifadhi
za Taifa, Hifadhi za Misitu na Maeneo Oevu na ujangili ukaanza kurejea. Aidha
watuhumiwa waliokuwa wametoroka kukimbia Operesheni wameanza kurejea kwenye
makazi yao.
Walivyoenguliwa;-
Ikiwa ni Desemba 2013, katika bunge lajamuhuri ya
muungano wa Tanzania, mawaziri Balozi Khamis Kagasheki wa maliasili.
Emmanuel
Nchimbi mambo ya ndani, waziri wa maendeleoya mifugoMathayo David, na waziri wa
mambo ya ndani mh Vuai Naodha, walilalamikiwa na bunge kuhusu utekelezaji wa
operation Tokomeza kuwa ilikuwa imekwenda kinyume.
Vitendo
vya Ukiukwaji Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu Rejea;
Tume imebaini kuwa katika
utekelezaji wa Operesheni kulikuwa na matukio ya ukiukwaji wa Sheria, Kanuni,
Taratibu na Hadidu Rejea. Ukiukwaji huu umesababisha madhara kwa wananchi
mbalimbali ikiwemo vifo, madhara ya mwili na kadhalika.
Tume ilichunguza matukio 15 ya
vifo.........
, na kuridhika kuwa vifo tisa (9) kati ya hivyo vilisababishwa na mateso ambapo watendaji kwenye Operesheni walitumia nguvu kubwa kupita kiasi dhidi ya watuhumiwa wakati wa ukamataji au kuhoji. Kabla ya vifo watu hao walikuwa chini ya ulinzi wa askari wa Operesheni na kuna ushahidi wa kitabibu (medical reports), ushahidi wa kimazingira na ushahidi wa kuona, unaohusisha vifo vya marehemu hao na mateso kutoka kwa askari wa Operesheni. Tume haikupata ushahidi wa kuhusisha vifo sita (6) vilivyobaki moja kwa moja na Operesheni Tokomeza.
, na kuridhika kuwa vifo tisa (9) kati ya hivyo vilisababishwa na mateso ambapo watendaji kwenye Operesheni walitumia nguvu kubwa kupita kiasi dhidi ya watuhumiwa wakati wa ukamataji au kuhoji. Kabla ya vifo watu hao walikuwa chini ya ulinzi wa askari wa Operesheni na kuna ushahidi wa kitabibu (medical reports), ushahidi wa kimazingira na ushahidi wa kuona, unaohusisha vifo vya marehemu hao na mateso kutoka kwa askari wa Operesheni. Tume haikupata ushahidi wa kuhusisha vifo sita (6) vilivyobaki moja kwa moja na Operesheni Tokomeza.
Tume ilichunguza madai ya mateso
yaliyosababisha madhara kwenye miili ya wahusika. Walalamikaji walieleza Tume
kwamba waliteswa ili waoneshe silaha au nyara zilipofichwa au wakiri
kujihusisha na ujangili au ujambazi na wataje washirika wao wa mtandao wa ujangili.
Kulikuwa pia na malalamiko ya udhalilishwaji. Malalamiko hayo yalitoka kwenye
wilaya ishirini na mbili (22) za mikoa mbalimbali. Yapo matukio ambayo
walalamikaji waliweza kuleta mbele ya Tume uthibitisho wa kuteswa, na
walionesha makovu na kutoa vyeti vya matibabu na PF 3 walizopewa baada ya
kuumia.
Tume imebaini kuwepo matendo
mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea uliofanywa
na baadhi ya askari wa Operesheni na maafisa wengine walioshiriki katika
utekelezaji wake, ikiwemo matukio yanayoashiria rushwa na udanganyifu
mbalimbali.
Tume ilishughulikia pia tuhuma za
wizi, upotevu na uporaji wa mali. Walalamikaji wa kundi hili walieleza Tume
kuwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni, waliibiwa au kupoteza fedha na mali
zao wakati na baada ya kukamatwa au kupekuliwa na askari wa Operesheni. Tume
ilichunguza jumla ya matukio ishirini na tatu (23) ya aina hiyo na kubaini kuwa
malalamiko mengi yalitokana na askari wa Operesheni kutofuata sheria, kanuni na
taratibu za ukamataji, kuhoji na upekuzi maungoni mwa watuhumiwa na kwenye
nyumba zao.
Kasoro zilizoonekana ni pamoja na
kutoshirikisha viongozi au watu huru katika upekuzi na kutojazwa hati za
upekuzi mara baada ya upekuzi. Kasoro nyingine ni askari wengi kuingia kwenye
nyumba kwa wakati mmoja. Aidha, Tume imebaini walalamikaji wengine waliongeza
chumvi katika ushahidi wao kuhusu idadi ya mali na fedha zilizopotea au kuibiwa
na hivyo ushahidi wao kutoaminika au kuthibitika.
Tume ilichunguza malalamiko ya
kubakwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni. Matukio yaliyochunguzwa na Tume
yalikuwa katika Kijiji cha Iputi, Wilaya ya Ulanga, Mkoa wa Morogoro na Kijiji
cha Mwantimba Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu na Wilayani Sikonge. Hata hivyo
wote waliodai kubakwa hawakujitokeza mbele ya Tume kutoa ushahidi wao, hivyo
Tume haikuweza kuchunguza malalamiko yao. Alijitokeza mlalamikaji mmoja
Wilayani Ulanga, Morogoro, lakini Tume haikuridhika na maelezo yake, ambayo
hayakutosheleza kubainisha kosa kwenye utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
Tume ilibaini kuwa wapo watuhumiwa
waliofikishwa mahakamani na kutiwa hatiani na wengine kuachiwa. Tume imeona
kuwa hatua hii ilikuwa sahihi kisheria. Lakini Tume ilibaini pia kuwa baadhi ya
watuhumiwa hawakufikishwa mahakamani. Badala yake maafisa wa Operesheni
walijichukulia mamlaka ya kutoa adhabu kwa watuhumiwa kama vile kukamata na
kuzuia mali zao, kuchoma moto nyumba na mali zilizokuwa kwenye maeneo ya
hifadhi, kuua au kujeruhi mifugo iliyokutwa kwenye maeneo ya hifadhi au kuuza
kwa mnada ng’ombe waliokamatwa kwenye maeneo ya hifadhi. Hatua nyingine
inayolalamikiwa ni kuchukua bunduki zinazomilikiwa kisheria.
Tume imebaini kwamba katika baadhi
ya maeneo askari wa Operesheni walichoma nyumba moto kwa madai ya nyumba hizo
kujengwa kwenye hifadhi. Malalamiko hayo yalitoka katika Wilaya za Mlele na
Mpanda, Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Mbeya; Wilaya za Nkasi na
Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa; na Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara. Katika
uchunguzi wa matukio haya Tume imebaini yafuatayo:-
.Wanakijiji hawakupewa taarifa ya
kutosha kuhamisha mali zao kabla ya kuchoma nyumba zao;
.Baadhi ya wanakijiji walipoteza
vyakula na mali zao katika zoezi hilo la uchomaji moto;
.Kuna vijiji vilivyosajiliwa lakini
sehemu ya vitongoji vyake viko ndani ya Hifadhi za Taifa;
.Kuna maeneo ya hifadhi au ushoroba
(buffer zone) ambayo hayana alama za mipaka kati ya hifadhi au ushoroba
na vijiji husika;
.Kuna nyumba ambazo hazikuwa kwenye
eneo la hifadhi au ushoroba na hivyo zilichomwa moto kinyume cha sheria.
.Baadhi ya matukio na malalamiko ya
kuchomewa moto nyumba yalitokea kabla ya Operesheni.
Uchunguzi wa Tume umebaini kuwepo
kwa tatizo kubwa la wafugaji kutoka nje ya nchi na wafugaji wenyeji kuingiza
mifugo yao katika Mapori ya Akiba, Hifadhi ya Misitu, Maeneo Oevu na Hifadhi za
Taifa. Maeneo yaliyoathirika sana na tatizo hili ni Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti, Pori la Akiba la Kigosi – Moyowosi, Pori la Akiba la Maswa, Mapori
ya Akiba ya Biharamulo – Burigi – Kimisi na Pori la Akiba la Kijereshi.
Katika baadhi ya maeneo
imethibitika kwamba wapo ng’ombe waliouawa kwa kupigwa risasi baada ya kukutwa
ndani ya hifadhi.
Aidha, Tume imeridhika kwamba kuna
ng’ombe wa walalamikaji waliokamatwa na kuuzwa kwa mnada. Uuzaji wa ng’ombe
katika tukio hili haukuzingatia utaratibu wa kisheria.
Tume ilipata ushahidi kwamba katika
maeneo mbalimbali askari wa Operesheni walikamata au kuchukua bunduki, risasi
pamoja na vitabu vyake hata kwa silaha zinazomilikiwa kihalali. Maeneo ambayo
yalikuwa na malalamiko ya watu kuchukuliwa silaha zao ni mikoa saba (7) ambayo
ni Katavi, Mbeya, Lindi, Morogoro, Tabora, Manyara na Pwani ambapo jumla ya
watu sitini na mbili (62) walijitokeza mbele ya Tume kulalamika tukio hili.
Hatua
Zitakazochukuliwa na Serikali;
Baada ya kupitia kwa kina taarifa
ya Tume, pamoja na mapendekezo ya Tume, Serikali itafanya yafuatayo:
Hatua za kimashtaka zitaendelea kwa
shauri la mauaji ambalo upelelezi wake umekamilika na hatua za kiuchunguzi
zitaendelea kwa mashauri mengine nane (8) ya mauaji ambayo upelelezi wake
haujakamilika;
.Hatua za kisheria na kiutawala
zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa waliothibitika kuwatesa watu 15 wakati wa
Operesheni;
.Hatua za kiuchunguzi zinazofanywa
na TAKUKURU kuhusu tuhuma za rushwa na udanganyifu zilizothibitika zitaendelea;
.Silaha zinazodaiwa kumilikiwa
kihalali zitafanyiwa uhakiki na ukaguzi wa kina kuhusu umiliki na matumizi yake
na endapo hakutakuwa na sababu nyingine za kisheria za kuzuia urejeshwaji,
wamiliki warejeshewe silaha zao kwa mujibu wa sheria na taratibu;-
.Mali ambazo zimethibitika
kuchukuliwa wakati wa Operesheni kwa tuhuma za kuhusishwa na uvunaji haramu wa
mazao ya misitu zirejeshwe endapo hakutakuwa na sababu za kisheria kuendelea
kuzishikilia, na itaangalia utaratibu wa fidia kwa wahusika.
Serikali itafanya uhakiki wa vijiji
ambavyo vimesajiliwa na vimo ndani ya hifadhi ili kutatua migogoro ya ardhi
kati ya hifadhi na vijiji. Aidha, Serikali itahakikisha kunakuwa na ushirikiano
wa karibu kati ya Msajili wa vijiji au mamlaka husika na Wizara ya
Maliasili na Utalii ili kuepuka kusajili vijiji ndani ya maeneo ya hifadhi;
Wizara ya Maliasili na Utalii
itatayarisha kanuni zitakazoweka utaratibu wa kuwaondoa watu waliovamia na
kujenga makazi katika hifadhi;
Sheria zote zinazolinda maeneo ya
hifadhi zitafanyiwa marekebisho ili kuongeza adhabu kwa kosa la kuingiza mifugo
kwenye Hifadhi bila kujali uraia wa wamiliki wa mifugo hiyo;
Kwa vile Tume imejiridhisha na
faida kubwa na mafanikio ya Operesheni Tokomeza, Serikali
itaendelea na Operesheni kama hizo kadri
itakavyojitajika ili kuokoa maliasili za Taifa, ikiwemo
wanyama, hifadhi na misitu. Hata hivyo ushauri wa Tume
juu ya kuboresha upangaji, usimamizi na utekelezaji wa Operesheni hizo
itazingatiwa kikamilifu.
Hadidu
Rejea kwa Tume;
.Kuchunguza namna Operesheni
Tokomeza ilivyotekelezwa;
.Kuchunguza iwapo maafisa
waliotekeleza Operesheni Tokomeza walizingatia sheria, kanuni, taratibu na
hadidu rejea walizopewa;
.Kuchunguza iwapo maafisa
waliotekeleza Operesheni Tokomeza walivunja sheria, kanuni, taratibu na hadidu
rejea walizopewa;
.Kuchunguza iwapo kuna watu
waliokiuka sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na iwapo
hatua zilizochukuliwa na maafisa wa Operesheni Tokomeza dhidi ya wakosaji hao
na mali zao zilikuwa sahihi;
.Kupendekeza hatua zinazostahili
kuchukuliwa dhidi ya maaafisa wa Operesheni Tokomeza waliokiuka sheria, kanuni,
taratibu na hadidu rejea za Operesheni Tokomeza; na
.Kupendekeza mambo yanayopaswa
kuzingatiwa katika kupanga na kutekeleza Operesheni nyingine kama hii ili
kuzuia na kuepuka malalamiko mengine kama yaliyotokea kwenye Operesheni
Tokomeza.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es
Salaam.
Mei, 2015


No comments:
Post a Comment