MAC PRODUCTION STUDIO'S

MAC PRODUCTION STUDIO'S
KWA MATANGAZO YA BIASHARA REDIONI( 0767-814844)

Monday, 1 June 2015

HOFU KUZAGAA WAKIMBIZI TANZANIA MAREKANI YATUA KUPUNGUZA ELFU TATU



Wakimbizi waliorejeshwa nchini Burundi kutoka kambi ya Mtabila iliyofungwa rasmi Desemba 2012 mkoani Kigoma, wameingia tena nchini na kujazana katika makazi ya muda ya Nyarugusu wakiomba hifadhi.

Mkuu wa Kambi ya Nyarugusu Sospter Christopher amemweleza hayo waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi aliyekwenda kuangalia hali halisi ya kambi ya Nyarugusu na Wakimbizi baada ya kutajwa kuwa wameanza kusambaa mitaani,  akiambatana na Maofisa wa Umoja wa Mataifa akiwemo Mratibu wa mashirika ya kimataifa hapa nchini Alvaro Rodriguez.

Kurejea kwa wingi kwa Wakimbizi hao ni pigo kisaikolojia kwa watu ambao walirejeshwa nyumbani kwa kuonekana kwamba hali ni shwari na walikuwa wameanza kuishi maisha ya kawaida.
Idadi hiyo ikichanganyika na wengine inafanya  kambi kuelemewa na kuonekana haja ya kutafuta eneo jingine la kupiga kambi kwa ajili ya Wakimbizi hao ambao wanaanza kwenda mitaani kwani mpaka mwishoni mwa wiki iliyopita walikuwa zaidi ya elfu 51.
“ Kwa sababu tunapokea idadi kubwa ya waomba hifadhi toka Burundi, tumekuwa tukiongeza idadi ya vituo vya mapokezi ili kukidhi mahitaji ya kuwapokea  wakati tukisubiri maelekezo toka ngazi za juu za kuwahamishia Migunga Hills eneo linalopendekezwa kufunguliwa kambi ya Nyarugusu B” alisema Christopher mbele ya Waziri Chikawe.
Alisema walianza kupokea waomba hifadhi hapo kambini kuanzia Aprili 29, 2015 kwa idadi ndogo kabisa ya watu 36, lakini idadi hiyo ilianza kuongezeka siku hadi siku na kufikia Mei 27 mwaka huu idadi yao ilifikia 48,333, idadi kubwa ikiwa wanawake na watoto.

Wakimbizi hao walikuwa wakipitia vituo vya Kigoma (27,638), Manyovu (4,439), Kilelema (1,603) na Kigadye (1,291).

Kambi hiyo yenye uwezo wa kubeba watu 50,000 imeelemewa kwa sababu ya ujio mpya uliosababisha kuwepo kwa Wakimbizi zaidi ya 106,410.

Kuna matatizo zaidi ya milipuko ya wagonjwa kambi hii imechanganywa na  Wakimbizi wa Kongo watu ambao hawana utamaduni wa pamoja na kuonekana hatari ya kukabiliana kwa kutosikilizana.

 Aidha kambi hiyo pamoja na kuwahifadhi waburundi wapo pia Wakimbizi kutoka Kongo wapatao 54,706; Burundi,3261 ; Rwanda 72; Uganda 17; Sudan Kusini wanane; Kenya 7; Somalia 3; Ethiopia 1; Zimbabwe 1; na Ivory coast 1.

Akijibu  maswali ya waandishi wa habari walioambatana naye katika ziara hiyo kuhusu hali ya baadae ya Wakimbizi wa Kongo ambao wapo nchini kwa takribani miaka 19 sasa, Waziri Chikawe alisema kwamba serikali haina mpango wa kuwapa uraia kwa sasa ingawa Marekani imesema itawachukua Wakimbizi elfu 30 kuwapeleka kwao na kwingine duniani.
“hatuna mpango wa kuwapa uraia kwa sasa na kuondolewa kwa hao  wengine kutasaidia kupunguza idadi yao katika kambi hiyo.
Ni lengo la serikali kuhakikisha kwamba kambi hiyo inapunguzwa ili kuweza kuchangia ipasavyo kwa hali bora ya Wakimbizi na kwamba mchakato wa kuwaangalia waomba hifadhi kama wanafaa kuwa Wakimbizi unaendelea.
Siyo kweli kuwa kuna watu hawajapata chakula kwa siku saba la sivyo wangelikufa.
Wakimbizi hawa wengi ni watoto na kwamba wanapoingia nchini wanapewa vyakula vikavu (kama biskuti)  lakini wakishafika kambini wanapewa chakula kilichopikwa na resheni ya siku 14 .
Wataalamu wanaangalia barabara mbadala kwani iliyopo sasa pamoja na kuhitajika milioni 300 kuitengeneza lakini bado kila mvua itakapokuwa inanyesha itahitaji kutengenezwa.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mtaifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole katika mahojiano na waandishi wa habari aliishukuru serikali ya Tanzania kwa kufungua mipaka ili Wakimbizi waweze kuingia na kutoa eneo kwa ajili ya kambi mpya kutokana na ya sasa kujaa sana.

Aidha aliishukuru serikali ya Uingereza kwa kuwa ya kwanza kutoa misaada kwa ajili ya Wakimbizi hao na kutarajia nchi nyingine kama Marekani itafanya hivyo mapema ili kuisaidia serikali ya Tanzania katika kuhudumia waomba hifadhi.

Naye Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Alvaro Rodriguez amesema wanafanya kila linalowezekana ili kupunguza idadi ya Wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu kwa kuwapatia eneo jingine la kujihifadhi.

Alisema kwa kuwatoa hapo watasaidia shule zilizofungwa ambazo zinasomesha watoto kutoka kwa Wakimbizi wa Kongo kurejea madarasani kukamilisha mtaala wao.

Na Modewjiblog team, Kigoma

No comments: