
Ni jengo la wodi ya wagonjwa mahututi
(Intensive Care Unit) katika hospitali ya rufaa mkoa Kagera litakalokuwa
likitoa huduma kwa wagonjwa mahututi bila kujali jinsi kutokana na uhitaji
wake, ambapo wananchi wamekuwa wakikosa huduma hiyo na kutajwa kupoteza maisha
hata kama ingewezekana wakatibiwa.
Akikagua jengo hilo ambalo limefikia
asilimia 99% katika ujenzi wake katibu tawala wa mkoa Kagera Bw. Nassor Mnambila Bw. Mnambila
alisema kuwa serikali ya mkoa iliamua kujenga jengo hilo la wagonjwa mahututi
ambalo hapo mwanzo halikuwepo na wagonjwa mahututi kukosa huduma ya sehemu
maalum ya uangalizi wa karibu na kusababisha usumbufu mkubwa kwao ambapo
amesisitiza likamilishwe kwa muda uliopangwa ili lianze kutumika na kutoa
huduma kwa wananchi.
Aidha akiongea na uongozi wa hospitali
hiyo Bw. Mnambila alitoa changamoto kwao kuwa sasa ni wakati wa serikali
kushirikiana na sekta binafsi katika kutekeleza miradi ya maendeleo inayowagusa
wananchi moja kwa moja badala ya kuitegemea serikali tu ambapo aliwashauri kuandika
maadiko ya miradi mbalimbali na kuiuza kwa sekta binafsi na mashirika
yasiyokuwa ya serikali.
Kutokana na maeneo ya hospitali hiyo
kuonekana kuwa finyu kwasababu ya kujenga majengo mbalimbali ya chini
aliwashauri kuona uwezekano wa kujenga majengo ya kwenda juu ambayo ni
maghorofa kwasababu itafika mahali hakuna tena sehemu ya kujenga jengo lolote
kutokana na ufinyu wa ardhi.
Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. Thomas
Rutachunzibwa akimshukuru Katibu Tawala Mkoa Bw. Mnambila alisema anamshukuru
yeye binafsi na serikali kwa ujumla kuona umuhimu wakujenga jengo la wagonjwa mahututi katika
Hospitali ya Rufaa ya mkoa na kupunguza usumbufu waliokuwa wanaupata, lakini
mara baada ya jengo hilo kukamilika litaondoa tatizo hilo.
Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera
inawahudumia wastani wa wagonjwa 12,000 kwa mwezi na wastani wa wagonjwa
150,000 kwa mwaka ambapo mwaka 2013 iliwahudumia wagonjwa 151,915 na mwaka
uliofuata iliwahudumia wagonjwa 156,376. Lengo kubwa la Sekretarieti ya mkoa wa
Kagera ni kutoa huduma nzuri kwa wananchi wake.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment