MULEBA
Baadhi ya wananchi wa kata Mayondwe wilayani Muleba wamejawa na taharuka baada ya kuibuka hali ya kushangaza kufuatia nyumba zao kuteketea ghafla kwa moto mchana kweupe pasipo kujua chanzo cha moto huo.
Diwani wa kata Mayondwe iliyopo wilayani humo Method Bakuza
amesema kuwa matukio ya nyumba kuteketea kwa moto wa ghafla yalianza may 4
mwaka huu katika kitongoji cha Ibila kijiji Bugasha ndani ya kata hiyo ambapo
kufikia leo zimeteketea nyumba 12 ndani ya kitongoji hicho na haijulikani
chanzo cha moto huo ni nini.
Aidha amesema kuwa moto huo unatokea muda wa mchana na
unateketeza nyumba pamoja na migomba inayokuwa jirani huku akiongeza kuwa
hakuna madhara yoyote yaliyotokea kwa binadamu labda mali zinazokuwa ndani ya
nyumba zinaungua kabisa maana moto unakuwa mkali kiasi kwamba wanashindwa
kuzima.
Kwa upande wake mmojawapo wa mashuhuda Jovenary Anatory
amesema kuwa nyumba ya kaka yake ni
miongoni mwa nyumba zilizoungua na walikuwa ndani ya nyumba hiyo lakini moto
umezuka ghafla na unaanzia kwenye paa na kuteketeza nyumba nzima.
MWISHO.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment