WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema salfa iliyoingizwa
nchini kwenye makontena 211 haina kasoro na inafaa kwa matumizi ya kupulizia
kwenye mikorosho.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Juni 10, 2017) wakati
akizungumza na wajumbe wa kamati maalum, waagizaji wa salfa na baadhi ya
wajumbe wa Bodi ya Korosho nchini (CBT) kwenye kikao alichokiitisha kwenye
makazi yake, Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
“Bodi kaandaeni taratibu za kawaida kusambaza salfa kwa
wakulima ili waanze kupuliza dawa hiyo. Wasichelewe kupuliza kwa sababu msimu
umeshaanza,” amesema.
Juni 4, mwaka huu Waziri Mkuu alimuagiza Mkemia Mkuu wa
Serikali, Prof. Samuel Manyele aende kuchunguza mzigo wa salfa ulioko bandari
ya Dar es Salaam baada ya kutokea mkanganyiko uliosababishwa na ripoti ya TPRI
kuwa ya salfa iliyoingizwa nchini na kampuni ya ETG Inputs Ltd kwa niaba ya
Bodi ya Korosho haijakidhi viwango.
Waziri Mkuu alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa kuna
mkanganyiko miongoni mwa wakulima juu ya matumizi ya kiuatilifu hicho licha ya
kuwa Serikali ilikwishapokea taarifa ya bodi, na taarifa ya kampuni
iliyotengeneza salfa hiyo na taarifa iliyoletwa na mwagizaji ambayo imethibitishwa na makampuni matatu ya kimataifa. Aliyataja makampuni hayo matatu kuwa ni InterTech, Bureau Veritas na SGS.
iliyotengeneza salfa hiyo na taarifa iliyoletwa na mwagizaji ambayo imethibitishwa na makampuni matatu ya kimataifa. Aliyataja makampuni hayo matatu kuwa ni InterTech, Bureau Veritas na SGS.
Akitoa taarifa ya uchunguzi wao mbele ya Waziri Mkuu, Prof.
Manyele alisema walifanya uchunguzi kwenye makontena 21 ambayo ni sawa na
asilimia 10 ya makontena yote 211 ili kubaini ubora wake.
“Uchunguzi ulifanyika kwenye maeneo ya purity, acidity
na moisture contents kama ulivyokuwa umeelekeza. Sampuli zilichukuliwa
kutoka GALCO Inland Container Depot iliyoko Chang’ombe ambako ndiko mzigo wa
salfa ulioletwa na kampuni ya ya ETG Inputs Ltd unahifadhiwa,” alisema.
“Kwa kuzingatia matokeo ya kiuchunguzi wa kimaabara
uliofanyika, viwango (specifications) vilivyowekwa ndani ya mkataba na viwango
vya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kuhusiana na kiuatilifu cha
salfa ni maoni yetu kuwa mzigo wa salfa ulioko ndani ya makasha (containers)
211 unakidhi viwango,” alisema kwenye taarifa yake.
Kwa upande wake,
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho nchini, Bw. Maokola Majogo alisema yeye
pamoja na Bodi yake watatekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu na akawataka wakulima
wasisite kutumia salfa hiyo kwani imekwishathibitishwa na Mkemia Mkuu kwamba
haina matatizo.
Naye, Kaimu
Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho nchini, Bw. Hassan Jarufu alisema Bodi iliagiza
salfa kwa kiwango kile kile cha mwaka jana kilichotumiwa na wakulima na kuleta
matokeo mazuri.
“TPRI walichukua sampuli na kuleta majibu kuwa ina mapungufu,
kwa hiyo tukashindwa kuisambaza. Mheshimiwa Waziri Mkuu alimuagiza Mkemia Mkuu
afanye uchunguzi wake, na sisi tumefurahia matokeo na tunaenda kutekeleza
maelekezo yake ya kututaka tusambaze salfa kwa wakulima,” alisema.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment