Wafamasia
nchini wametakiwa kuzingatia maadili na weledi katika kutekeleza majukumu yao
ili kuchochea azma ya Serikali ya Awamu
ya Tano kutoa huduma bora za afya kote nchini hali itakayochea maendeleo na
ukuaji wa sekta hiyo.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Msajili wa Baraza la Famasi nchini Bi.
Elizabeth Shekalaghe wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wafamasia
waliohitimu masomo yao hivi karibuni katika vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya
nchi na kula kiapo cha kuzingatia maadili ya taaluma hiyo adhimu kwa
mustakabali wa ukuaji wa sekta ya afya hapa nchini.
“Mafunzo
haya yamehusisha takribani wafamasia 160 na yanalenga kuwakumbusha wajibu wao na
umuhimu wa kuzingatia maadili na kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza
wakati watakapokuwa wanatekeza majukumu yao kwa kuwa wapo watakafanya kazi
katika Mikoa, Halmashauri na Hospitali katika maeneo mbalimbali “ alisisitiza
Shekalaghe.
Akifafanua
amesema kuwa mafunzo hayo yameshafanyika
katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,Kaskazini,Mashariki na Kanda ya Ziwa
dhamira ikiwa kuwajengea uwezo wafamasia wanaohitimu kabla ya kuanza kutekeleza
majukumu yao mara baada ya kula kiapo.
Aliongeza
kuwa jukumu la Baraza hilo ni kufuatilia mwenendo wa wafamasia ili kuhakikisha
kuwa wanazingatia maadili ya taaluma hiyo na wamiliki wa maduka ya dawa
kuhakikisha kuwa wanaajiri wafamasia wenye sifa na waliosajiliwa ili watoe
huduma bora kwa mujibu wa sheria na kanuni.
Kwa
upande wake Naibu Msajili wa Baraza hilo Bi. Zainabu Nyamungumi akiwasilisha
mada katika mafunzo hayo amesisitiza umuhimu wa wafamasia kufanya kazi kwa
kuzingatia sheria na taratibu zinazosimamia taaluma hiyo katika maeneo
watakayokuwa wanafanya kazi.
Pia
aliwataka kutekeleza kwa vitendo yale waliyofundishwa katika mafunzo hayo ili
kuchochea ukuaji wa taaluma hiyo.
Naye
mdau wa Taaluma hiyo ambaye pia ni mwanataaluma Bw. Manase Kejo iliwataka
wafamasia hao kujiamini na kujiajiri kwa kuwa taaluma waliyo nayo ni fursa inayoweza
kuzalisha ajira.
“Ni muhimu mkatambua kuwa taaluma hii ni muhimu na
jambo kubwa ni kutambua kuwa mnaweza kujiajiri,” Alisisitiza Kejo.
Mwaka 2013 Tanzania ilikuwa na wafamasia takribani
450 na kufikia mwaka 2017 wamefikia 1600 hali inayoonyesha kuwa taaluma hiyo inaendelea
kukua kwa kasi suala linalochagizwa na ongezeko la vyuo vinavyotoa taaluma hiyo kikiwemo Chuo
Kikuu cha Mtakatifu John Dodoma, Bugando na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment