WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi
mkoani Songwe, Bw. Eliseyi Mgoyi pamoja na maofisa wengine watatu kwa
tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.
Pia amemuagiza Kamanda wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Songwe, Bw. Damian
Sutta kuwakamata na kuanza kuwachunguza haraka maofisa hao na kisha
ampelekee taarifa ofisini kwake.
Waziri Mkuu amewasimamisha kazi
maofisa hao leo (Jumapili, Julai 23, 2017) wakati alipozungumza na
watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwenye ukumbi wa Shule ya
Sekondari Vwawa, akiwa katika ziara yake ya kikazi.
Maofisa wengine waliosimamishwa
kazi ni pamoja na Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo ni Bw.
Simon Noel, Bw.
Bahati Chomoka ambaye ni Cashier na Bw. Remmy Haule ambaye ni Ofisa
Ugavi.
Waziri Mkuu amesema Maofisa hao
wamekiuka sheria za matengenezo ya magari ya Serikali kwa kwenda
kutengeneza katika gereji ambazo hazikusajiliwa na wala hazifanyi
shughuli hiyo, jambo ambalo halikubaliki.
Amesema Kampuni ya Umbwila ni
moja kati ya Kampuni zinazolipwa fedha nyingi za utengenezaji wa magari
ya Halmashauri ya wilaya ya Mbozi huku ikiwa haina sifa za kufanya kazi
hiyo ya utengenezaji magari.Kampuni zingine ni Julius Diesel, Kasaba na
Mtoni Garage.
“Mfano duka la Umbwila ambalo
linauza vipuri vya magari lakini Halmashauri inalilipa fedha kwa ajili
ya utengenezaji wa magari jambo ambalo si sahihi kwa sababu lile ni duka
la vipuri na si gereji. Wanamlipa muuza vipuri kama mtengeneza magari”.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa
“hatuwezi kuendesha Serikali kwa namna ambayo haikubaliki kwani watu
tuliowapa dhamana ndio wanaongoza kwa vitendo vya rushwa na ufisadi.
Wameifanya Halmashauri hii kama shamba la bibi”.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu
amemtaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mheshimiwa Eric Ambakisye
kuhakikisha anasimamia vizuri utendaji ndani ya Halmashauri hiyo na
kwamba Serikali inataka watu waadilifu na wenye uaminifu na nidhamu.
“Halmashauri inanuka rushwa
tunataka iwe safi. Hatuwezi kukubali kuona Halmashauri hii na zingine
nchini zikigeuzwa kuwa magenge. Kwa Serikali hii no, hatuhitaji rushwa
wala harufu ya ufisadi.”
Waziri Mkuu amesema Serikali
haiwezi kuvumilia kuona watumishi waliopewa dhamana wakijinufaisha kwa
fedha za umma na kuwaacha wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa
huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za maji, afya na elimu, hivyo
itaendelea kuwachukulia hatua.
Pia Waziri Mkuu amewataka
Madiwani na Wakuu wa Idara katika Halmashauri zote nchini wabadilike na
wahakikisha wanashirikiana na kufanya kazi kwa ushirikiano kwani
wakigawanyika watashindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia
wananchi
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment