Afisa msajili wa vitambulisho vya taifa NIDA, ambaye sasa
yupo mkoani Kagera kusimamia uandikishaji katika manispaa ya Bukoba Bi. Sophia
Mfinanga, amesema kuwa hakuna ulazima wa
vitambulisho hivyo, kwasababu kinachoendelea sasa ni utambuzi na uandikishaji
wa wananchi katika daftari la kudumu la makazi.
Ameagiza watendaji wa kata, mitaa kutokuwazuia wananchi
wanaojitokeza kuandikishwa, na mwananchi hatakiwi kuondoka na fomu hiyo, badala
yake ijaziwe hapohapo kwenye ofisi za kata au mtaa chini ya uangalizi wa
mtendaji au mwenyekiti.
Amesema kuwa mamlaka ya vitambulisho vya taifa NIDA, tarehe
30/05/2017 ilitoa elimu yaani mafunzo elekezi kwa wenyeviti wa mitaa na ilitoa
mafunzo kwa watendaji mitaa na kata ikiwa ni tarehe 9/06/2017, hivyo uandikishaji utaendelea hadi 15/07/2017,
na hakuna kuwazuia kuandika kwa kukosa cheti cha kuzaliwa, viapo pamoja na
vitambulisho vingine kama leseni, kadi ya mpiga kura au vyeti vya shule, kwani
kama kutakuwa na lazima hiyo wataelekezwa na maofisa wa uhamiaji.
Siku
chache zilizopita, Mtendaji wa kata ya Bakoba katika manispaa ya Bukoba na
wengine watatu, wameshikiliwa na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa
TAKUKURU mkoani Kagera, kwa kuwatoza wananchi shilingi elfu tano katika
uandikishaji wa vitambulisho vya taifa.
Akizungumza
na mwandishi wa mtandao huu, mkuu wa Takukuru mkoani Kagera Joseph Mwaiswelo, alisema
kuwa pamoja na kukamatwa kwa mtendaji
huyo, pia inawashikiria watu watatu na wanaendelea kuhojiwa.
Alimtaja
mtendaji huyo kuwa Marco Mgoe, huku akisisitiza kuwa majina ya wengine
yanahifadhiwa kwa sababu za uchunguzi, na kuwa wanatuhumiwa kwa kutoza wananchi
shilingi elfu tano kwa ajili ya kupewa fomu za vitambulisho vya taifa wakati wa
uandikishaji unaoendelea.
Na Mwanaharakati.