TATIZO la Tanzania la kuuza bidhaa nje na kushindana katika
Soko la Kimataifa limetatuka baada ya sasa kuwa imeingia katika mfumo wa
kimataifa wa utambuzi wa bidhaa kwa kutumia Nembo za Mistari (Bar Code).
Hayo yalifahamika wakati
Waziri Mkuu Mizengo Pinda
anazindua mpango mkakati wa miaka mitano wa taasisi inayosimamia nembo
hiyo nchini Global Standard One (GS1) – Tanzania National Ltd., kwenye ukumbi
wa Blue Pearl Hotel, Ubungo jijini Dar es Salaam leo (Jumatano Feb. 27, 2013)
mchana.
Namba ya utambulisho ya nembo hiyo kwa Tanzania ni 620 na
tayari imeunganishwa katika mtandao wa GS1 duniani. Mpaka sasa wazalishaji 370
wa bidhaa mbalimbali wamekwishapata na wanatumia nembo hiyo wakiwa na jumla ya
bidhaa 6,000 sokoni.
“Hili ni jambo jema. Bado nina imani kwamba tunaweza kufanya
vizuri zaidi na kupiga hatua kubwa zaidi
kama tukidhamiria. Changamoto ninayoiona sasa ni jinsi ya kutangaza mafanikio
hayo ambayo tayari tumeyafikia,” Pinda alisema.
Waziri Mkuu aliitaka GS1 Tanzania, kutumia matangazo ya
Televisheni, kushiriki katika Maonyesho ya Kilimo na Nane Nane na Maonyesho ya
Kimataifa ya Biashara kutangaza nembo hiyo ili wazalishaji wengi zaidi
wajiungenayo.
GS1 ni Shirika la Kimataifa lisilo la kiserikali na lisilo
la faida lililoanzishwa mwaka 2005 na lenye makao makuu yake Brussels,
Ubelgiji. Shirika hilo limeisaidia Tanzania kuanzisha shughuli hiyo nchini,
miaka miwili iliyopita.
Kabla ya GS1 Tanzania, wazalishaji wa bidhaa wa Tanzania
walikuwa wanapata nembo Kenya na Afrika Kusini na kuonyesha kama vile bidhaa
hizo zinatoka katika nchi hizo.
Waziri Mkuu alisema kuanzishwa kwa GS1 Tanzania ni sehemu ya
matokeo ya nia ya serikali ya awamu ya nne kuhakikisha kuwa chombo hicho
kinaanzishwa nchini kama moja ya taasisi za viwango nchini.
Alisema nembo hiyo ni fursa nzuri kwa wazalishaji, hasa
wajasiriamali wadogo, kupenya kwenye soko la kimataifa na kupata biashara nzuri
na fedha nyingi.
Pinda aliliagiza Shirika la Viwango nchini TBS na Wakala wa
Usajili wa Makampuni na Leseni za Biashara, kutoa umuhimu wa kwanza kwa
wazalishaji wadogo wanapotaka kupatiwa nembo ya viwango na kusajili biashara.
“TBS muwe na kitengo cha wafanyabiashara wadogo na
wajasiriamali. Msiwachanganye hawa na wafanya biashara wakubwa, mtawabana sana
na watashindwa kunyanyuka,” alisema.
Katika sherehe hiyo, Waziri Mkuu alizindua mpango huo kwa
kukata utepe na kuanzisha king’ora. Pia litoa mfano wa nembo hiyo ya mistari
kwa wazalishaji mbalimbali.
Waziri Mkuu pia yeye mwenyewe alikabidhiwa nembo hiyo kwa
kuzalisha asali.
(mwisho)
Imetolewa na:
Ofisi ya
Waziri Mkuu,
S.L.P. 3021,
DAR ES
SALAAM